Wairani wajitokeza kwa wingi kuwaaga mashahidi wa shambulizi la kigaidi la Israel
Shughuli ya kuwaaga mashahidi wa shambulizi la kigaidi la Israel nchini Syria imefanyika hapa Tehran kwa kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi ya juu, familia za mashahidi hao na umati mkubwa wa wananchi Waislamu wa Iran.
Kwa mujibu wa IRNA, maelfu ya Wairani wamejitokeza kaskazini mashariki mwa Tehran kuwaenzi washauri hao wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) waliouawa shahidi karibuni nchini Syria.
Washiriki wa shughuli hiyo ya kuwaaga mashahidi hao wa Syria ambao ni Hojjatollah Omidvar, Ali Aqazadeh, Hossein Mohammadi, Saeed Karimi na Mohammad Amin Samadi wamesikika wakipiga nara za mauti kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na mauti kwa Marekani.
Kwa mujibu wa tovuti ya kanali ya Press TV, watatu kati ya mashahidi hao wanazikwa Tehran, na wengine wawili wanatazamiwa kuzikwa katika mji mkakatifu wa Qum, kusini mwa Tehran.
Washauri hao watano wa kijeshi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) waliuawa shahidi juzi Jumamosi katika shambulizi la kigaidi la anga lililofanywa na utawala wa Kizayuni huko Damascus, mji mkuu wa Syria.
Shambulio hilo lililenga jengo la makazi la orofa tatu katika kitongoji cha Mezza mjini Damascus ambalo lina nyumba kadhaa za wanadiplomasia wa kigeni.
Rais Ebrahim Raisi wa Iran amelaani vikali shambulizi hilo la kigaidi la Israel katika mji mkuu wa Syria, Damascus na kusisitiza kuwa, vitendo vya aina hiyo vya kioga haviwezi kupita hivi hivi bila kupewa jibu.