Marais wa Iran na Uturuki wasaini hati 10 za ushirikiano
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki zimetia saini hati 10 za ushirikiano kwa lengo la kuzidisha uwekezaji, ushirikiano wa kiuchumi na masuala ya kieneo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran (IRNA), hati hizo za ushirikiano zilitiwa saini usiku wa Jumatano katika uga wa utamaduni, vyombo vya habari na mawasiliano, usafiri wa reli na anga, umeme, nishati, maeneo ya biashara huria. Sherehe za kusainiwa hati hizo zilihudhuriwa na Marais wa Jamhuri ya Kiislamu, Sayyid Ebrahim Raisi na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki.
Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, aliwasili jana Ankara, mji mkuu wa Uturiki, kuhudhuria kikao cha Baraza Kuu la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Uturuki akiongoza ujumbe wa kiuchumi na kisiasa.
Baada ya kuwasili mjini Ankara, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikaribishwa rasmi na mwenzake wa Uturuki katika Ikulu ya Rais, Aksaray.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia alikuwa na kikao cha faragha na Erdogan kwa muda wa saa mbili katika Ikulu ya Aksaray mjini Ankara, kisha akashiriki katika kikao cha nane cha Baraza Kuu la Ushirikiano wa Iran na Uturuki.