Raisi: Visiwa 3 vya Ghuba ya Uajemi ni sehemu isiyotenganishika na Iran
Rais wa Iran amesema visiwa vitatu vinavyomilikiwa na nchi hii vya Bu Musa, Tomb Ndogo na Tomb Kubwa katika Ghuba ya Uajemi daima vitasalia kuwa milki ya Jamhuri ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Rais Ebrahim Raisi alisema hayo jana Alkhamisi akiwa katika ziara ya kikazi katika mkoa wa kusini wa Hormozgan na kuongeza kuwa, visiwa hivyo vinavyopatikana katika maji ya Ghuba ya Uajemi ni milki ya daima ya Iran na ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Kadhalika Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amevishukuru vyombo vya usalama vya nchi hii kwa kudhamini usalama na amani ya kudumu katika eneo la Asia Magharibi.
"Uwepo wa Iran katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman unadhamini usalama, lakini uwepo wa maajinabi unatishia amani ya eneo," ameongeza Sayyid Ebrahim Raisi.
Tehran inasisitiza kuwa, nyaraka za historia zenye itibari ya kimataifa zinathibitisha kuwa visiwa vitatu vya Bu Musa, Tomb Ndogo na Tomb Kubwa katika Ghuba ya Uajemi ni mali ya Iran.
Kwa mfano, ramani ya jeshi la majini la Uingereza mnamo mwaka 1881 inaonyesha ramani ya Wizara ya Masuala ya Bahari ya Uingereza ya mwaka 1863 na pia ramani ya Iran iliyochorwa na Wizara ya Vita ya Uingereza mwaka1886.
Katika ramani hiyo, visiwa hivyo vimepakwa rangi ya ardhi ya Iran, na kuna mifano ya hati za kimataifa zinazoonyesha mamlaka ya Iran kwa visiwa hivyo, ambavyo Imarati imekuwa ikidai ni vyake.