Kusambaratishwa mitandao ya kijasusi ya "Mossad" nchini Iran
Wizara ya Intelijensia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa imefichua vibaraka kadhaa wa shirika la ujasusi la Israel, Mossad katika nchi 28 duniani.
Katika taarifa yake ya jana Ijumaa, Wizara ya Intelijensia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitoa maelezo kuhusu mfululizo wa operesheni zake za hivi karibuni na kusema kwamba, kutokana na juhudi za mafisa wa taasisi hiyo, makumi ya majasusi na magaidi wenye mfungamano na shirika la ujasusi la Israel (Mossad) wametambuliwa katika nchi 28 za dunia katika mabara matatu ya Asia, Afrika na Ulaya.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, mashirika ya ujasusi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yalibuni mbinu mbalimbali na kutumia vibaya majukwaa ya umma kama intaneti, mitandao ya kijamii na tovuti zinazojihusisha na uhajiri na kutafuta ajira, yakijaribu kuwasiliana na wahanga kwa njia tofauti; na katika hatua zilizofuata, yalikusanya taarifa kutoka kwa wahanga hao au kuwapa majukumu ya kufanya uharifu.
Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran imeashiria pia katika taarifa hiyo historia na rekodi za majasusi waliotambuliwa na kueleza kwamba, baadhi yao walishirikiana na Mossad "kwa hiari" na kufanya uhaini dhidi ya nchi zao, na kwamba shirika hilo la ujasusi la Israel "liliwalazimisha" watu hao kutekeleza operesheni mbalimbali za kihaini dhidi ya maslahi ya nchi zao.
Habari hiyo ya kutambuliwa na kunaswa maajenti wa mashirika ya ujasusi ya Israel kutokana na taarifa na kazi kubwa ya vyombo vya upelelezi vya Iran, imetolewa huku idara za intelijensia na masuala ya usalama za Iran zikiwa zimetoa kipigo kikubwa kwa Mossad katika miaka miwili iliyopita. Kukamatwa kwa wanachama wa timu 6 za shirika la ujasusi la Israel, Mossad, katika mikoa tofauti ya Iran kwenye kipindi cha miezi kadhaa iliyopita kunatathminiwa katika mkondo huo. Mwezi Disemba mwaka jana pia, wanachama wakuu wanne wa timu ya hujuma yenye mfungamano na Mossad walinyongwa mkoani Azarbaijan Magharibi baada ya kupatwa na hatia ya kufanya vitendo vilivyo dhidi ya usalama wa nchi.
Ripoti zinaonyesha kuwa, kutambuliwa na kutiwa mbaroni majasusi wa utawala wa Kizayuni nchini Iran na katika nchi nyingine za eneo la Magharibi mwa Asia kumeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miezi ya hivi karibuni hususan baada ya vita vya Gaza, kiasi kwamba serikali ya Uturuki ilitangaza mwezi uliopita kwamba imenasa mitandao kadhaa ya kijasusi ya Mossad na kukamata baadhi wanachama wao. Majasusi wa Mossad waliokamatwa nchini Uturuki walikiri kwamba, walikuwa wakifanya mikakati ya kuwateka nyara baadhi ya watu na kutekeleza hujuma za kigaidi nchini Uturuki, kwa sababu ya uungaji mkono wa Ankara kwa mapambano ya watu wa Gaza na kwa lengo la kupindisha maoni ya umma kutoka kwenye mauaji ya kimbari yanayojiri sasa huko Gaza.
Duru mpya ya kuwabaini, kuwafichua na kuwatia mbaroni majasusi wa Mossad katika eneo la Magharibi mwa Asia na Iran inaonyesha kuwa, harakati za kijasusi na haribifu za utawala wa Kizayuni zimeongezeka katika eneo hilo, na utawala huo unajaribu kuendeleza malengo yake kwa kufanya uharibifu na mauaji ya kigaidi. Mauaji ya kigaidi ya makumi ya washauri wa kijeshi wa Iran na viongozi wa makundi ya Muqawama wa Palestina na Lebanon katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita yanatathminiwa katika mwelekeo huo. Hata hivyo, operesheni za hivi karibuni za maafisa wa upelelezi na usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya mipango na mitandao yenye mfungamano na Mossad zinaonyesha kuwa idara za usalama za Iran ziko macho na makini na zinafuatilia kwa karibu nyendo za majasusi wa Israel ndani na nje ya mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu, na kamwe hazitaruhusu kutekelezwa njama za adui Mzayuni na Marekani dhidi ya watu na maafisa wa Iran.
Katika upande mwingine, nchi zinazodai kupambana na ugaidi zinajaribu kuidhihirisha Iran na Mhimili wa Muqawama kuwa ndiyo sababu ya ukosefu wa usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia kwa kutoa tuhuma za uongo. Sasa inatupasa kusubiri na kuona iwapo harakati za kigaidi na kijasusi za Israel katika nchi za Magharibi mwa Asia zitalaaniwa na waungaji mkono wa utawala huo ghasibu au la.
Inatupasa kusema kuwa, tangu kuasisiwa utawala haramu wa Israel katika ardhi ya Palestina ambako kulifanyika kwa mashambulizi ya kigaidi, uvamizi na mauaji, maadui wa taifa la Iran wamekuwa wakitenda kwa mujibu wa malengo ya utawala huo haramu na kunyamaza kimya mbele ya uhalifu unaofanywa na Israel. Mfano wa wazi zaidi wa ukweli huo ni misimamo ya nchi za Magharibi hususan Marekani, Uingereza na Uujerumani mbele ya mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.