Iran yalaani mashambulizi ya Marekani na Uingereza nchini Yemen
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani mashambulizi ya anga na makombora ya Marekani na Uingereza dhidi ya miji na maeneo tofauti ya Yemen.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Naser Kan'ani Chafi amesema hayo leo hapa Tehran na sambamba na kulaani vitendo vya madola ya kiistikbari ya Marekani na Uingereza ya kutoheshimu mtawalia haki ya kujitawala taifa la Yemen amesema, kuendelea vitendo kama hivyo vya kiholela ni tishio kwa amani na usalama kwa dunia nzima.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, chokochoko za kijeshi za Marekani na Uingereza za kushambulia nchi tofauti za eneo hili ni muendelezo wa siasa potofu za madola hayo mawili ya kibeberu za kudhani kuwa zinaweza kudhamini maslahi yao haramu kwenye eneo hili kwa njia za kijeshi.
Amesema, mashambulizi hayo ya Marekani na Uingereza ni uvunjaji wa wazi kabisa wa haki ya kujitawala taifa na nchi huru ya Yemen na yanakinzana kikamilifu na madai ya mara kwa mara ya Washington na London kwamba eti hawapendi kuona eneo la Asia Magharibi linakumbwa na vita vikubwa.
Naser Kan'ani ameongeza kuwa, mashambulizi ya Marekani na Uingereza nchini Yemen ni kuonesha jinsi madola hayo ya kiistikbari yanavyounga mkono kikamilifu jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Palestina na hasa Ghaza na uvamizi wao huo wa kiijeshi katika nchi mbalimbali za eneo hili kama Iraq, Syria na Yemen unazidisha tu hali ya wasiwasi kwenye ukanda huu na hauwezi kuuokoa utawala pandikizi wa Israel.