May 05, 2024 12:23 UTC
  • Mottaki: Operesheni dhidi ya Israeli ilifichua 'sehemu ndogo ya uwezo wa Iran'

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Iran Manouchehr Mottaki anasema operesheni ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya Israel ilionyesha "sehemu ndogo" tu ya uwezo wa Iran wa kukabiliana na utawala huo ghasibu.

Katika mahojiano na kituo cha habari cha televisheni ya Iran cha Al-Alam siku ya Jumamosi, Mottaki alisema kuwa shambulio hilo lililopewa jina la Operesheni ya Ahadi ya Kweli, lilifanywa kwa kuzingatia mpango wa kina na sahihi.

Ameongeza kuwa operesheni hiyo iliyofanywa kujibu kitendo cha woga cha utawala wa Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus iliyopelekea kuuawa shahidi Wairani kadhaa, ilionyesha sehemu ndogo tu ya uwezo wa Iran wa kukabiliana na utawala wa Kizayuni,"

Mottaki, ambaye pia ni mbunge mteule, alisema kuwa operesheni ya Iran ilikuwa operesheni ya kwanza ya kuhujumu ya kijeshi ya Iran tangu baada ya muongo 1980 wakati wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran.

Vile vile amesema utawala wa Kizayuni pamoja na Marekani, Ufaransa na Uingereza zilishirikiana kukabiliana na operesheni hiyo ya Iran, lakini wanajeshi wake walitumia mbinu mbalimbali ili kukabiliana na adui na hivyo makombora yao yaliweza kushambulia na kulenga kwa nguvu shabaha zilizokusudiwa.

Ikumbukwe kuwa, Jumatatu, Aprili 1, 2024, utawala wa Kizayuni wa Israel ulishambulia ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus katika shambulio la kigaidi lililopelekea kuuawa shahidi washauri saba wakuu wa kijeshi wa Iran. Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran aliitaja hatua hiyo ya Israel kuwa shambulio dhidi ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni "utaadhibiwa." Katika kutekeleza ahadi hiyo, Jumapili asubuhi (tarehe 14 Aprili 2024), Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilichukua hatua ya kuuadhibu utawala huo wa Kizayuni kwa kuvurumisha ndege zisizo na rubani na makombora kuelekea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) kupitia operesheni ya kuiadhibu Israel iliyopewa jina la "Ahadi ya Kweli."