May 22, 2024 07:53 UTC
  • Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aongoza swala ya maiti ya mashahidi wa ajali ya helikopta

Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi ameongoza swala ya maiti na kuwaombea maghfira kwa Mwenyezi Mungu mashahidi Rais Sayyid Ebrahim Raisi na wenzake.

Siku ya Jumapili jioni Mei 19 helikopta iliyokuwa imewabeba Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wenzake aliokuwa amefuatana nao ilipata ajali na kuanguka  katika eneo la Varzghan katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki, kaskazini magharibi mwa Iran ilipokuwa ikirejea kutoka katika hafla ya ufunguzi wa bwawa la "Qiz Qalqis, na kupelekea kufa shahidi Rais Raisi, Hossein Amir Abdullahian Waziri wa Mambo ya Nje, Imam wa Ijumaa wa Tabriz, Gavana wa mkoa wa Azerbaijan mashariki na maafisa wengine waliokuwa katika msafara wa rais. 

Mazishi ya mashahidi wa ajali ya helikopta nchini Iran 

Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi ameongoza swala ya maiti kwa shahidi Raisi na wenzake katika Chuo Kikuu cha Tehran.  

Marasimu ya ibada ya mazishi ya mashahidi hawa tajwa yameanza leo mapema asubuhi hapa Tehran  kwa kusoma aya za Qurani Tukufu. Shughuli hiyo imehudhuriwa na idadi kubwa ya wananchi, wakuu wa mihimili mitatu ya dola, viongozi mbalimbali, maafisa wa serikali na jeshi kwa kusoma aya za Quran Tukufu. 

Miili ya mashahidi wa ajali ya helikopta iliondolewa katika Chuo Kikuu cha Tehran na kupelekwa na wananchi waumini katika uwanja wa Azadi baada ya swala ya maiti iliyoongozwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.