Wagombea wa urais Iran wabainisha mipango yao kwenye mdahalo wa kwanza
(last modified Tue, 18 Jun 2024 03:26:28 GMT )
Jun 18, 2024 03:26 UTC
  • Wagombea wa urais Iran wabainisha mipango yao kwenye mdahalo wa kwanza

Mdahalo wa kwanza wa wagombea urais nchini Iran ulifanyika jana usiku kupitia televisheni ya taifa, na kuendelea kwa muda wa karibu saa nne.

Kila mgombea alipewa muda wa kutosha wa kueleza sera na mipango yake iwapo atachaguliwa na wananchi, kupitia kujibu maswali ya wananchi, wataalamu na waandishi wa habari. Mdahalo wa jana ulijikita zaidi katika masuala ya uchumi, diplomasia na ushirikiano wa kimataifa.

Wawaniaji hao wa kiti cha rais walibainisha kwa kina ajenda, sera na mipango yao iwapo wataibuka na ushindi katika uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika Juni 28. 

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad Baqer Qalibaf ambaye anaongoza katika utafiti wa maoni amesema, serikali inapasa kuhakikisha kuwa matatizo ya kiuchumi yanapatiwa ufumbuzi kupitia ushirikiano wa wananchi na wawekezaji.

Naye Saeid Jalili ambaye ni mjumbe mkuu wa zamani wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran amesema iwapo atachaguliwa kuliongoza taifa, atahakikisha kuwa anavutia uwezekaji kama njia kuu ya kuimarisha ustawi wa uchumi wa nchi.

Midahalo ya wagombea urais hapa nchini ni kielelezo cha sera ya Jamhuri ya Kiislamu ya kuwa na uwazi kwa wanachi. Midahalo mingine minne inatazamiwa kufanyika katika siku zijazo, huku wa mwisho ukiratibiwa kufanyika Juni 25, siku tatuu kabla ya uchaguzi. 

Wagombea sita akiwemo Jalili na Qalibaf wameidhinishwa na Baraza la Kulinda Katiba kuwania urais katika uchaguzi wa rais wa kabla ya wakati wa Juni 28. Wengine ni Alireza Zakani, Mostafa Pourmohammadi, Massud Pezeshkian, na Amir-Hossein Qazizadeh Hashemi.

Kura hiyo iliitishwa baada ya Rais Ebrahim Raisi kufa shahidi katika ajali ya helikopta akiwa na watu wengine saba mnamo Mei 19, katika mkoa wa Azerbaija Mashariki, kaskazini-magharibi mwa Iran.

Tags