Iran: Muqawama lazima uifanye Israel ilipe gharama kubwa kwa uvamizi
Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema makundi ya muqawama yanapasa kutumia nguvu na uwezo wao wote kuufanya utawala wa Kizayuni wa Israel ulipe gharama kubwa kutokana na uvamizi na mashambulizi yake dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran alisema hayo jana Alkhamisi katika mazungumzo yake mjini Doha, Qatar na Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS.
Ameeleza bayana kuwa, mapambano dhidi ya Wazayuni na waungaji mkono wao hayapasi kuishia tu ndani ya ardhi ya Palestina dhidi ya vikosi vamizi vya utawala haramu wa Israel na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuunga mkono muqawama kwa hali na mali.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa, sanjari na kuendeleza mapambano ya silaha, lakini muqawama unapasa kuchukua pia mielekeo na sura nyinginezo kama za kisheria, kisiasa na kidiplomasia nje ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, kwa shabaha ya kupigania na kutetea haki za Wapalestina.
Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran aidha amesema kuwa, Wazayuni kwa kufanya mauaji dhidi ya Wapalestina wanataka kurejea katika hali yao ya kabla ya tarehe 7 Oktoba 2023, lakini hali ya mambo haitarejea kama ilivyokuwa kabla ya hapo.
Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kwa upande wake amesema kundi hilo la muqawama katu halitasalimu amri, bali litaendeleza mapambano yake kwa nguvu zote.
Sambamba na kuishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa misaada na uungaji mkono wake usio kikomo na mipaka kwa HAMAS, ameeleza kuwa, harakati hiyo itaendeleza mapambano hadi ipate ushindi kamili dhidi ya Wazayuni maghasibu.
Haniya ameashiria mapendekezo kadhaa yaliyotolewa kuhusu usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza na kueleza kuwa, HAMAS inakaribisha mkakati au mpango wowote ambao utakidhi matakwa ya taifa la Palestina.