Iran itarusha satelaiti zaidi katika anga za mbali hivi karibuni
Mkuu wa Wakala wa Anga za Mbali nchini Iran Hassan Salarieh ametangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itarusha angalau satelaiti 6 katika anga za mbali kabla ya mwisho wa mwaka huu wa Kiirani.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano asubuhi, Salarieh alitoa muhtasari wa mafanikio yaliyopatikana katika maendeleo ya mpango wa anga za mbali wa Iran na akaeleza mipango iliyotekelezwa na wakala huo tangu mwaka huu wa Kiirani wa 1403 hadi sasa.
Amesema katika miaka mitatu iliyopita, miradi kuhusu miundombinu ya tasnia ya anga za mbali nchini Iran ilianzishwa na kukamilika. Amesema moja ya miradi mashuhuri zaidi ni kituo cha anga za mbali cha Chabahar kusini mwa Iran.
Ameongoza kuwa, kabla ya mwisho wa mwaka huu wa Kiirani utakaomalizika Machi 20 2025, awamu ya kwanza ya kituo cha anga cha Chabahar kitaanza kufanya kazi.
Mkuu wa Shirika la Anga la Iran ameendelea kusema kuwa Iran itarusha angani satelaiti 6 hadi 8 kufikia mwishoni nwa mwaka mpya wa Kiirani.
Sekta ya anga za mbali inazingatiwa kuwa kati ya tasnia zenye teknolojia ya hali ya juu. Pamoja na kuwepo vikwazo vya madola hasimu ya Magharibi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kumiliki mzunguko kamili wa teknolojia ya anga za juu. Hii ina maana kuwa, mbali na kuwa na uwezo wa kuunda na kurusha satalaiti angani, Iran pia ina kituo cha ardhini cha kupokea data zinazotumwa na satalaiti zilizoko angani.
Hivi sasa Iran ni miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza duniani katika sekta ya anga za mbali na mafanikio hayo ni matokeo ya zaidi ya miongo 4 ya jitihada za wataalamu wa nchi hii ya Kiislamu.