Kamanda Salami: Muqawama utalipiza kisasi cha jinai za karibuni za Israel
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) amesema jinai za hivi karibuni za Israel katika eneo la Asia Magharibi zimechochea moto wa ghadhabu miongoni mwa wapiganaji wa makundi ya muqawama ambao sasa wana azma thabiti ya kulipiza kisasi mkabala wa utawala wa Kizayuni.
Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa SEPAH alisema hayo jana Alkhamisi katika ujumbe wa kumuenzi mshauri wa kijeshi wa Iran, Milad Bidi, ambaye ni miongoni mwa wahanga wa operesheni ya umwagaji damu ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Beirut, mji mkuu wa Lebanon.
Salami amempongeza mshauri huyo aliyeuawa shahidi Beirut, kwa juhudi zake kubwa za kuyatetea Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa Iran, na vile vile kwa jitihada zake za kulinda usalama na amani ya nchi mkabala wa njama za maadui.
Milad Bidi aliuawa shahidi siku ya Jumanne wakati shambulio la kigaidi la Wazayuni lilipolenga jengo alilokuwa akiishi Fuad Shukr, mmoja wa makamanda wakuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.
Kamanda huyo mwandamizi wa Hizbullah ya Lebanon, pamoja na mshauri wa kijeshi wa Iran, Milad Bidi, waliuawa shahidi Jumanne wakati droni ya Israel iliporusha makombora matatu katika nyumba waliyokuwamo katika eneo moja karibu katika kitongoji cha Haret Hreik.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran amesisitiza kuwa, hasira na hamu ya kulipiza kisasi jinai za hivi karibuni zilizofanywa na utawala wa Kizayuni vimeongezeka katika eneo zima.