Aug 10, 2024 10:36 UTC
  • Amir Saeid Iravani
    Amir Saeid Iravani

Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu katika Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, haki ya kujilinda kuhusiana na mauaji ya Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas mjini Tehran haina uhusiano wowote na usitishaji vita huko Gaza na kusema kuwa, usitishaji vita katika eneo la Magharibi mwa Asia ni kipaumbele cha Iran.

Akijibu swali kuhusu iwapo Iran itaakhirisha jibu lake kwa utawala wa Israel baada ya mauaji ya Ismail Haniyeh, kiongozi wa Hamas akiwa mjini Tehran, hadi baada ya mazungumzo ya wiki ijayo kuhusu usitishaji vita huko Gaza, Amir Saeid Iravani, mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa alisema Ijumaa iliyopita kwamba masuala hayo ni vitu viwili tofauti, na haki ya Iran ya kujilinda haina uhusiano wowote na usitishaji vita huko Gaza. Iravani aliongeza kuwa, kuhusu usitishaji vita, makubaliano yoyote yatakayokubaliwa na Hamas na wananchi wa Palestina yatakubaliwa pia na Iran. Iravani amesema: "Usalama wa taifa letu na mamlaka ya kujitawala vimekiukwa katika kitendo cha karibuni cha kigaidi cha utawala wa Israel, na kwa sababu hiyo tuna haki halali ya kujilinda."

Amir Saeid Iravani

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas na mpatanishi mkuu wa harakati hiyo katika mazungumzo ya kusitisha mapigano, Ismail Haniyeh, aliuawa shahidi Jumatano Julai 31, akiwa katika makazi alikokuwa amefikia mjini Tehran. Baada ya kuuawa shahidi kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Hamas akiwa ugenini mjini Tehran, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kuwa utawala wa kigaidi wa Israel na waungaji mkono wake wanahusika na kitendo hicho cha kigaidi. Viongozi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni umevuka mstari mwekundu wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kumuua shahidi Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas akiwa mjini Tehran, na kusisitiza kuwa Iran itajibu jinai hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 51 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unajaribu kukwamisha mazungumzo ya kusitisha vita huko Gaza kwa kumuua Ismail Haniyeh, aliyekuwa mpatanishi mkuu wa harakati ya Hamas katika mazungumzo hayo. Katika miezi kadhaa iliyopita, utawala wa Kizayuni daima umekuwa ukikwamisha mazungumzo ya usitishaji vita kwa kutumia visingizio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa matakwa yasiyo na mantiki na kuzidisha mauaji ya raia wa Gaza ili kufikia malengo yake ya kisiasa na kijeshi katika ardhi za Palestina. Wakati huo huo, waungaji mkono wa Kimagharibi wa Israel hususan Marekani, kwa upande mmoja wanadai kuunga mkono mazungumzo ya usitishaji vita huko Gaza, na kwa upande mwingine wanaendelea kuupa utawala huo silaha zenye haribifu mkubwa kwa lengo la kuzidisha mauaji ya kimbari ya Wapalestina katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.

Gaza

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na televisheni ya Israel, asilimia 54 ya Wazayuni wanaamini kuwa malengo ya kisiasa ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ndiyo sababu ya kutositishwa vita vya Gaza. Kupitia njia ya kurefusha vita huko Gaza, Netanyahu anajaribu kutimiza ahadi zake, ikiwa ni pamoja na kuiangamiza kikamilifu Hamas, kambi ya Muqawama na kudhibiti usalama wa eneo hilo la Gaza.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeendelea kutilia mkazo utekelezwaji wa matakwa halali ya watu wa Palestina. Kuondoka wavamizi eneo la Gaza na kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika makazi yao ni miongoni mwa masharti makuu ya Hamas katika mchakato wa mazungumzo ya usitishaji vita. Kwa kutilia maanani yanayojiri katika uwanja wa vita vya Gaza, inapaswa kufahamika kuwa makundi ya Muqawama ya Palestina yataendeleza mapambano hadi matakwa yao halali yatakapotimizwa, na hadaa na uongo wa utawala wa Kizayuni na muungaji mkono wake mkuu, serikali ya Marekani, hautaathiri mchakato wa mazungumzo ya kusitisha mapigano.

Katika hali hiyo, hapana shaka kwamba, kusaidia kuimarisha amani na utulivu wa eneo la Magharibi mwa Asia ni moja ya vipengele muhimu vya siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na Tehran inaendelea kufanya juhudi zake zote ili kufanikisha suala hilo. Sambamba na hayo, utawala wa Kizayuni na wa kibaguzi wa Israel unaoendelea kufanya mauaji ya kimbari na kuibua mgogoro kwa kuwaua kwa umati watu wa Gaza na viongozi wa muqawama ndani na nje ya ardhi za Palestina.

Tags