Qalibaf: Israel haielewi lugha nyingine isipokuwa ya mabavu
(last modified Sun, 11 Aug 2024 07:33:46 GMT )
Aug 11, 2024 07:33 UTC
  • Qalibaf: Israel haielewi lugha nyingine isipokuwa ya mabavu

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imedhamiria kujibu mapigo kwa Israel kufuatia mauaji ya kigaidi ya Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS hapa Tehran akisisitiza kuwa, utumiaji wa nguvu na mabavu ndiyo njia pekee ya kukabiliana na Uzayuni.

Mohammed Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran amesema hayo leo mwanzoni mwa kikao cha Bunge na kusisitiza kwamba, "Utawala wa Kizayuni ambao ni fedheha kwa ubinadamu, haufahamu kitu kingine chochote isipokuwa lugha ya mabavu."

Huku akiyataja majibu ya Iran kwa mauaji ya Haniyah kuwa wajibu wa kidini na kitaifa kwa Iran, Qalibaf amesisitiza kuwa, Wazayuni wanapasa kujiandaa kwa adhabu kali na ya kuumiza ya Iran. Amebainisha kuwa, Iran itatoa jibu kali ambalo litamfanya adui na waungaji mkono wake wajute na kutothubutu tena kufanya kosa la kijinga kama hilo.

Qalibaf ameashiria shambulio la Jumamosi asubuhi dhidi ya shule ya Tabieen huko Gaza na kueleza kuwa, linaonyesha namna msingi wa utawala huo wa Kizayuni ulivyojengwa kwa kutegemea vitendo vya mabavu na ubaguzi; na wakati huo huo unadhihirisha namna utawala huo usivyoheshimu kanuni na sheria za kimataifa.

Ukatili wa Israel huko Gaza

Spika wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni unaelewa tu lugha ya mabavu, na serikali za Kiislamu lazima zichukue hatua za kivitendo za kuzuia mauaji ya kimbari yanayofanywa na Wazayuni, na kuweka kando kauli na matamshi hewa. 

Amesema uungaji mkono wa serikali za Magharibi kwa Israel, hasa Marekani, unahimiza utawala huo kuendelea na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Tags