Iran: Israel haitaweza katu kufidia vipigo vya kushindwa ilivyopata tangu Kimbunga cha Al-Aqsa hadi sasa
Aug 12, 2024 03:09 UTC
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, licha ya jinai na mauaji ya kutisha uliyofanya dhidi ya Wapalestina, Utawala wa Kizayuni wa Israel hautaweza katu kufidia vipigo vya kushindwa kistratejia ulivyopata tangu ilipotekelezwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa hadi sasa.
Nasser Kanani Chafi, ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kuwa, mauaji ya halaiki na ya kutisha ya Wapalestina yaliyofanywa kila mahala na wakati yamewadhihirishia walimwengu wote dhati ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni, sura halisi ya waungaji mkono wasio na utu wa utawala huo katili, na uwongo wa kaulimbiu za kutetea haki za binadamu zinazotolewa na Marekani na baadhi wanaojidai hivyo pia huko Ulaya.
Kanani Chafi amesisitiza kuwa, kushadidi unyama na ukatili wa utawala wa Kizayuni, unaofanywa kwa uungaji mkono wa moja kwa moja na wa kila hali wa Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi, ni ishara ya hofu uliyonayo utawala huo bandia ya kuporomoka na kusambaratika.
Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Iran ameongeza kuwa, nafasi ya kupumua utawala wa Israel katika eneo na duniani inazidi kuwa finyu siku baada ya siku, hasira za walimwengu dhidi ya utawala huo zinazidi kuwa kubwa, hali ya kukata tamaa ndani ya jamii na kwa wasomi wa utawala ghasibu wa Israel inazidi kuzigubika nyoyo zao na hofu ya mustakabali wa wingu na giza wa utawala huo na wakazi wake walowezi inazidi kuongezeka.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza bayana kuwa, ushindi katika vita hivyo visivyo na mlingano ni wa taifa la Palestina lenye asili, historia na chimbuko katika ardhi ya Palestina. Inachopasa kuliambia taifa linaloteseka na lenye majonzi lakini lenye subira na istikama la Palestina ni kwamba, vumilieni kidogo tu, mapambazuko ya asubuhi yanakaribia.../