Aug 15, 2024 07:43 UTC
  • Baadhi ya Wairani kwenda Arubaini, Iraq kwa njia ya bahari

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefungua njia ya baharini kutoka Bandari ya Khorramshahr, Magharibi mwa Iran hadi Bandari ya Basra nchini Iraq kwa ajili ya safari ya majini ya Mazuwari wa Kiirani wanaoenda kushiriki Arubaini ya Imam Hussein AS.

Iran Press imeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, safari ya majaribio imefanyika kutathmini usafiri huo wa baharini, ili Wafanyaziara wa Iran waweze kusafiri kwa njia ya bahari kwenda kushiriki katika matembezi hayo makubwa ya kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein, mjukuu wa Mtume Muhammad SAW aliyeuawa kidhulma mjini Karbala mwaka 61 Hijria.

Kufikia sasa Mazuwari 230 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesafiri kwenda Basra (Bandari ya Al Maqal) nchini Iraq kupitia usafiri huo wa baharini.

Wananchi wa Iran wamekuwa wakisafiri hadi Iraq kwa mabasi, treni na ndege, na sasa njia ya baharini imefunguliwa kuwahudumia Mazuwari hao. Njia hiyo ya baharini kati ya nchi hizi mbili imefunguliwa baada ya miaka 25. 

Kwa muda wa siku kadhaa zilizopita, Wafanyaziara kutoka nchi kadhaa zikiwemo Iran, Afghanistan, Pakistan, Jamhuri Azerbaijan, Bahrain, Kuwait na Saudi Arabia wamekuwa wakiwasili Karbala, iliyoko takriban kilomita 100 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Usimamizi wa Haram ya Hadhrat Abbas AS, watu zaidi ya milioni 22 walishiriki katika Arubaini ya Imam Hussein AS ya mwaka jana 2023. Mjumuiko wa Arubaini huko Karbala Iraq, unatajwa kuwa mjumuiko mkubwa zaidi wa kidini ulimwenguni, unaowaleta pamoja mamilioni ya wafanyaziara kutoka mataifa mengi duniani.

Tags