Iran yaionya Israel isikichezee Kibla cha Kwanza cha Waislamu
(last modified Wed, 28 Aug 2024 06:54:38 GMT )
Aug 28, 2024 06:54 UTC
  • Iran yaionya Israel isikichezee Kibla cha Kwanza cha Waislamu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa onyo kwa utawala wa Kizayuni na hasa serikali ya hivi sasa ya watenda jinai ambayo imepanga njama za kikhabithi dhidi ya Msikiti wa al Aqsa ambao ndicho Kibla cha Kwanza cha Waislamu ikiwaambia Wazayuni wasilichezee eneo hilo takatifu.

Nasser Kan'ani amesema hayo katika mtandao wa kijamii wa X na kuandika: Baraza la Mawaziri la utawala mtenda jinai wa Kizayuni, lina nia chafu ya kujenga sinagogi katika Msikiti wa al Aqsa bila ya hata kuona aibu, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwanza inalaani vikali mpango huo na pili inaionya Israel isivuuke mistari myekundu ya umma wa watu bilioni mbili wa Waislamu duniani. 

Amesema, mbali na kuamka fikra safi na za kimaumbile za watu wengi duniani na kuongezeka chuki na hasira dhidi ya jinai za Wazayuni, leo hii Waislamu na wapenda haki kote ulimwengu, wanaliunga mkono kwa kauli moja taifa la Palestina na Msikiti wa al Aqsa na wanalaani jinai za Wazayuni kwa sauti kubwa.

Itamar Ben Gvir, waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni mwenye misimamo ya kufurutu ada na chuki za kupindukia dhidi ya Waislamu, hivi karibuni alitangaza kuwa ana nia ya kuubomoa Msikiti wa al Aqsa na kujenga hekalu la Kizayuni.

Msikiti wa al Aqsa ni miongoni mwa maeneo matakatifu sana kati ya Waislamu wote duniani. Ndicho Kibla cha Kwanza cha Waislamu kabla ya Makkah na uko katika mji wa Baytul Muqaddas huko Palestina. Wazayuni wanafanya njama za kila namna za kutaka kuuvunja Msikiti huo.