Sep 08, 2024 08:10 UTC
  • Mkuu wa IRGC: Iran ililenga meli 12 za Israel baada ya meli zake za mafuta kulengwa

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Meja Jenerali Hossein Salami amefichua kuwa Iran ilizilenga kwa mafanikio meli kumi na mbili za Israel baada ya utawala huo kulenga meli za mafuta za Iran katika maji ya kimataifa.

Amesema: "Wao (Waisraeli) walilenga meli zetu 14 ili kusimamisha usafirishaji wa mafuta ghafi nje ya nchi. Awali, hatukujua ni nani hasa aliyehusika na mashambulizi hayo kwani yalikuwa yakiendeshwa kwa njia isiyoeleweka. Hatimaye, tuligundua kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel ndio ulikuwa mhusika na hivyo tukalenga meli zake 12."

Akizungumza Jumamosi wakati akiwa na Rais Masoud Pezeshkian katika Makao Makuu ya Ujenzi ya Khatam al-Anbiya katika mji mkuu Tehran, Jenerali Salami ameongeza kuwa: "Mara tu meli yao ya tano ilipogongwa, waliinua mikono yao juu na kutoa wito wa kusitishwa vita vya meli,"

Amesema wakati Uingereza ilipokamata meli ya mafuta ya Iran katika eneo la Gibraltar mwaka 2019, Iran nayo ilichukua udhibiti wa meli yao ya Stena Impero na hivyo wakasalimu amri na kurejesha meli ya Iran.

Aidha amebaini kuwa wakati maadui pia waliteka meli ya mafuta ya Iran huko Ugiriki, Iran nayo katika kujibu mapigo ilichukua meli mbili za maadui na hivyo wakasalimu amri na kurejesha meli ya Iran. Salami alikuwa akiashiria hatua ya kulipiza kisasi ya Iran mnamo Mei 2022 wakati meli ya mafuta ya Iran ilitekwa na Marekani kwenye pwani ya Ugiriki.

Stena Impero

Jenerali Salami amesema kuwa Iran ilikuwa inapitia kipindi kigumu sana wakati huo kwani kamanda mkuu wa Iran wa kupambana na ugaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa ameuawa shahidi katika shambulio la kigaidi la ndege isiyo na rubani ya Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, janga la COVID-19 lilikuwa limeenea nchini, vikwazo vya kiuchumi vilikuwa vimefikia kiwango cha juu kabisa na maadui walikuwa wakijaribu kuitenga kabisa Jamhuri ya Kiislamu.

Ameongeza kuwa IRGC ilitumia uwezo wake wote kutengeneza chanjo ya virusi vya COVID-19 ndani ya nchi, kupunguza mdororo wa kiuchumi uliosababishwa na janga la COVID-19, kulinda njia za meli, kubatilisha vikwazo na kupambana na tishio la magaidi wakufurishaji waliokuwa wakifadhiliwa na madola ya kigeni.