Sep 17, 2024 13:17 UTC
  • Sisitizo la Kiongozi Muadhamu la ulazima wa umoja wa Umma wa Kiislamu

Kwa miaka mingi, umoja wa ulimwengu wa Kiislamu ni miongoni mwa masuala makuu na ya kimsingi ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amekuwa akiyasisitizia kila mara katika miongozo na jumbe zake kwa kuwapa nasaha wanachuoni, wasomi, viongozi wa kisiasa na Umma wa Kiislamu juu ya ulazima wa kuunda umoja wa jamii na serikali za Kiislamu.

Jumatatu ya jana Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alilisisitiza tena umuhimu wa umoja wa Umma wa Kiislamu alipokutana na Maulamaa, Maimamu wa Swala ya Ijumaa pamoja na wakurugenzi wa Madrassa za Waislamu wa madhehebu ya Suni kutoka kote Iran kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Umoja wa Kiislamu sambamba na siku za kukumbuka kuzaliwa mbora wa viumbe Mtume Muhammad (SAW).

Ayatullah Khamenei amesema katika kikao hicho kwamba, kuna udharura wa kulinda utambulisho wenye thamani wa 'Umma wa Kiislamu' na kusisitiza kuhusu umoja wa Kiislamu. Huku akiashiria njama za wasiowatakia mema Waislamu ambao wanavuruga umoja huo amesema: "Kadhia ya Umma wa Kiislamu haipaswi kusahauliwa."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: "Suala la utambulisho wa Umma wa Kiislamu ni jambo la kimsingi ambalo linavuka utaifa na mipaka ya kijiografia." Amesisitiza kuwa, uhakika na utambulisho wa umma wa Kiislamu haubadiliki."

Ayatullah Khamenei ameashiria njama za mahasimu za kuwafanya Waislamu wapuuze au wasijali kuhusu utambulisho wao wa Kiislamu na kuongeza kuwa: "Ni kinyume cha mafundisho ya Kiislamu wakati Mwislamu anapoghafilika kuhusu masaibu ya Waislamu wenzake huko Gaza na maeneo mengine duniani."

Hapana shaka kwamba ulimwengu wa kiistikbari wa leo umechukua msimamo mmoja wa chuki dhidi ya dini ya Kiislamu, kiasi kwamba unajaribu kuwagawa Waislamu wa dunia kwa kutangaza uwongo na kuutukana Uislamu na familia ya Mtukufu Mtume (SAW).

Kiongozi Muadhamu katika mazungumzo yake na Maulamaa na wanazuoni wa Kisuni 16/09/2024

 

Katika kipindi hiki hasasi na nyeti, ulazima wa kuwepo umoja baina ya Waislamu unaonekana zaidi kuliko wakati mwingine wowote, na kwa msingi huo, serikali za Kiislamu hazipaswi kuwaruhusu maadui kuutenganisha na kuusambaratisha Umma ulioungana wa Kiislamu kwa kueneza fakachi na mifarakano.

Kwa hiyo, wiki ya umoja inachukuliwa kuwa fursa nzuri ya uelewa na umoja wa kalima (neno) na kuondokana na njama za maadui.

Uzoefu wa miongo ya hivi karibuni unaonyesha wazi kwamba, maadui daima wamejaribu kuzuia uhuru wa kweli na mamlaka ya kujitawala Waislamu, na katika hali hii, wanatumia njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na propaganda mbaya za vyombo vya habari dhidi ya Waislamu, kueneza chuki dhidi ya Uislamu, kuwatuhumu Waislamu kwa itikadi kali na ugaidi pamoja na kuleta mgawanyiko miongoni mwa wafuasi wa madhehebu mbalimbali.

Kuhusiana na hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka wanazuoni wa Kisuni kuegemea utambulisho wa Kiislamu na Umma wa Kiislamu na akaashiria miundo na shughuli za kihistoria mbaya ya watu wenye nia mbaya kwa ajili ya kuchochea hitilafu za kidini katika ulimwengu wa Kiislamu hususan nchini Iran na kubainisha kwamba, "Kwa kutumia nyenzo za kifikra, kipropaganda na kiuchumi, wanataka kuwatenganisha Shia na Sunni katika nchi yetu na eneo lolote la Kiislamu, na wanachochea kufurutu ada na mifarakano kwa vitendo kama vile kuwalazimisha watu wa pande zote mbili kusemana vibaya."

Kiongozi Muadhamu akisaliimiana na mmoja wa wanazuoni wa Kisuni

 

Ni wazi kwamba Waislamu watakapokuwa wamegawanyika, hawataweza tena kufikia malengo yao matukufu ikiwa ni pamoja na uhuru na maendeleo ambapo badala ya kuelekeza nguvu zao kwenye mambo yenye utata na yasiyo na matunda, wanapaswa kuelekeza nguvu zao kwenye masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu.

Ni dhahiri kuwa, kinachodhoofisha malengo maovu ya maadui na ubeberu katika ulimwengu wa Kiislamu na kukwamisha maslahi yao bila shaka ni umoja wa Waislamu na pia kuzingatia kwa dhati suala muhimu zaidi la hivi sasa la ulimwengu wa Kiislamu yaani Palestina ambalo limesisitizwa mara nyingi na kiongozi mkuu wa mapinduzi ya Kiislamu.

Katika matamshi yake ya jana, Ayatullah Khamenei alibainisha kuwa, ili kufikia lengo muhimu la izza na heshima ya Umoja wa Kiislamu hakuna njia nyingine isipokuwa kwa umoja na akasema: "Leo moja ya mambo ya wajibu yasiyo na shaka kamili ni kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa wa Gaza na Palestina, na mtu ye yote akiasi wajibu huu, bila shaka ataulizwa swalii hilo na Mwenyezi Mungu.