Iran: Israel lazima iwajibishwe kwa jinai ya kigaidi iliyofanya Lebanon
Sep 18, 2024 06:58 UTC
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amelaani ugaidi wa kimtandao uliofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Lebanon na kusema: Utawala wa Kizayuni lazima uwajibishwe kwa uchokozi na jinai hiyo ya kutisha.
Hizbullah ya Lebanon ilitangaza katika taarifa iliyotoa siku ya Jumanne (Septemba 17, 2024) kuwa: vifaa kadhaa vya kupokea ujumbe vya "Pagers", ambavyo vilitumiwa na idadi kubwa ya wafanyakazi wa vitengo na taasisi mbalimbali za harakati hiyo, viliripuliwa kupitia hujuma kigaidi iliyofanywa na utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi punde ya Wizara ya Afya ya Lebanon, watu 11 wameuawa shahidi na wengine 2,750 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo ya kigaidi.
Kuhusiana na suala hilo, Amir Saeed Iravani, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelaani jinai hiyo alipohutubia kikao cha dharura cha Baraza Kuu la umoja huo kilichofanyika jana na kusisitiza kuwa, utawala ghasibu wa Israel unapaswa kuwajibishwa kwa jinai hiyo ya kutisha.
Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, naye pia amesema, kitendo hicho cha kigaidi dhidi ya raia ni kinyume cha kanuni zote za kimaadili na kiutu, sheria za kimataifa hususan sheria za kimataifa za kibinadamu na akataka kufunguliwa mashtaka kimataifa ya jinai, kupandishwa kizimbani na kuadhibiwa wahusika wa uhalifu huo.
Stefan Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa, yeye amesema anatiwa wasiwasi na yanayojiri nchini Lebanon, hasa kwa kuzingatia hali "tete mno" inayotawala katika nchi hiyo.
Jinai hiyo ya kigaidi ya kimtandao iliyofanywa na utawala wa Kizayuni imelaaniwa imelaaniwa pia na Waziri Mkuu wa Iraq Muhammad Shia al-Sudani, Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria na maafisa kadhaa waandamizi wa Yemen akiwemo msemaji wa Harakati ya Ansarullah Muhammad Abdussalam.../