Oct 09, 2024 13:59 UTC
  • Ismail Baqaei
    Ismail Baqaei

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amejibu madai ya afisa wa usalama wa Uingereza akisema: Maafisa wa serikali ya London wanapaswa kutumia ushawishi wao kusimamisha uchokozi na jinai za utawala ghasibu wa Israel badala ya kutoa tuhuma zisizo na msingi na mijadala ya kupotosha.

Ni baada ya Ken McCallum, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ujasusi wa Ndani ya Uingereza (MI5), kudai jana Jumanne bila kutoa ushahidi wowote, kwamba tishio la Daesh (ISIS) limerejea na kwamba Iran na Russia pia zinapanga njama na hujuma nchini Uingereza!

McCallum pia alidai kuwa kufufuliwa kundi la ISIS nchini Afghanistan kumepelekea kuanza tena jitihada za kundi hilo (la kigaidi) za kusambaza ugaidi, na kwamba idadi ya raia wa Uingereza wanaotaka kusafiri nje ya nchi kujiunga na kundi hilo "imeongezeka kwa kiasi fulani".

Ismail Baqaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekanusha kabisa madai ya afisa huyo wa usalama wa Uingereza dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kulaani kukaririwa madai hayo katika miaka miwili iliyopita, ambayo yanatolewa bila hata chembe ya ushahidi.

Amesema, tuhuma za taasisi za usalama za Uingereza dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinazotolewa katika fremu ya kutengeneza "uadui" bandia na kupotosha maoni ya umma kuhusu nafasi na machango wa London katika kuendeleza mauaji ya kimbari ya Wapalestina na uchochezi wa vita wa utawala wa Kizayuni katika eneo la Magharibi mwa Asia.GaGa

Israel, kisaidiwa na nchi za Magharibi kama Marekani na Uingereza, inaendeleza mauaji ya kimbari huko Gaza

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amewashauri maafisa wa serikali  ya London kwamba, wanapaswa kutumia ushawishi wao kukomesha mashambulizi na jinai za utawala ghasibu wa Israel badala ya kutoa shutuma zisizo na msingi na kuibua mijadala ya kupotosha.

Pia, ameashiria hatua ya London ya kuwa mwenyeji wa baadhi ya makundi na mashirika ya kigaidi ambayo yanaendeleza ukatili na ugaidi kwa mpangilio maalumu na kueneza chuki kwa kutumia vibaya dhana ya uhuru wa kujieleza, na kukumbusha wajibu wa kisheria wa kimataifa wa nchi zote wa kukabiliana na ugaidi na uchochezi wa machafuko.

Tags