Iran yataka kutumiwa uwezo wa eneo kukomesha mauaji ya halaiki
(last modified Thu, 10 Oct 2024 12:23:58 GMT )
Oct 10, 2024 12:23 UTC
  • Iran yataka kutumiwa uwezo wa eneo kukomesha mauaji ya halaiki

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ametoa mwito wa kutumika kwa uwezo na suhula zote za eneo la Asia Magharibi ili kusimamisha vita mara moja na kuzuia kuendelea mauaji ya kimbari na uharibifu wa miundo mbinu huko Lebanon na Palestina.

Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo mjini Doha katika mazungumzo yake na Sheikh Muhammad bin Abdul-Rahman al-Thani, Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar na kusisitiza udharura wa kuhitimishwa jinai na mauaji ya kiimbari ya utawala haramu wa Israel.

Akiashiria sera ya ujirani mwema na maendeleo ya pande zote ya mahusiano na majirani kuwa ni kipaumbele muhimu cha serikali ya 14 ili kufikia amani, utulivu, usalama pamoja na maendeleo na ustawi wa kieneo, Araghchi ameutathmini uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Qatar kuwa ni wa kidugu na wenye kuimarika na kusisitiza juu ya utekelezaji wa makubaliano ya awali kati ya nchi hizo mbili.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar na Iran

 

Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar pia ametilia mkazo juu ya kuendelezwa uhusiano wa karibu na wa kirafiki kati ya Qatar na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kupanuliwa uhusiano huo katika azma na irada ya viongozi wa nchi hizo mbili.

Katika upande mwingine akizungumza na kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar kwamba, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu kwa muqawama na kusema kuwa, uungaji mkono wa Iran hautakuwa tu wa kisiasa na wa kidiplomasia na kamwe hautaacha muqawama huo.

Tags