Pezeshkian, Putin wapongeza uhusiano wa ‘kimkakati’ kati ya Iran na Russia
Rais Vladmir Putin wa Russia amemwambia Rais mwenzake wa Iran, Masoud Pezeshkian kwamba uhusiano na Iran ni kipaumbele kwa Russia na uhusiano huu sasa unaendelea kwa mafanikio.
Marais hao wawili walikutana kando ya kongamano katika mji mkuu wa Turkmenistan, Ashgabat, siku ya Ijumaa, ambapo Putin alisema misimamo ya Tehran na Moscow kuhusu matukio ya kimataifa inakaribiana sana.
Kiongozi wa Russia amesema: "Moscow na Tehran zinashirikiana kikamilifu katika nyanja ya kimataifa na mara nyingi hukubaliana juu ya tathmini zao za matukio ya ulimwengu." Pezeshkian alisema uhusiano wa Iran na Russia ni "wa dhati na wa kimkakati".
Rais wa Iran amegusia makubaliano ya kina ya ushirikiano wa kimkakati kati ya Iran na Russia, akitumai hatua za utiaji saini wa waraka huo zitaharakishwa.
Rais Pezeshkian pia ameashiria matukio katika eneo la Asia Magharibi, ikiwa ni pamoja na ukatili wa Israel dhidi ya watu wa Palestina na Lebanon. Amesema: "Utawala wa Kizayuni hauheshimu mfumo wowote wa kisheria na kibinadamu wa kimataifa, na hali katika eneo ni mbaya."
Mkutano huo wa Ashgatat umeudhuriwa na viongozi wengine wa kanda akiwemo Rais wa Pakistani Asif Ali Zardari na wakuu wa mataifa mengine ya Asia ya Kati ambaye ni Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan na Uzbekistan.
Akizungumza wakati kongamano hilo lilipofunguliwa, Rais Putin alisema nchi hizo zinataka kuunda "utaratibu mpya wa dunia" ili kukabiliana na madola ya Magharibi.