Iran: Walimwengu wachukue hatua kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, walimwengu wanapaswa kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na hatua za kishari na jinai za utawala haramu wa Israel.
Ismail Baqaei sambamba na kulaani shambulio la askari wa utawala ghasibu kwa mabavu dhidi ya Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa (UNIFIL) nchini Lebanon amesema, shambulio dhidi ya askari hao wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa ni mfano mwingine wa uvunjaji sheria na ujeuri wa uwepo ambao katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita umeua zaidi ya wafanyakazi 220 wa Umoja wa Mataifa huko Gaza.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameashiria vitendo vya kifidhuli vya viongozii wa Israel kama hatua ya balozi wake ya kuchana hati ya Umoja wa Mataifa; Waziri wake wa mambo ya nje kumtambulisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kama kipengele kisichofaa na hatua ya waziri mkuu wake mpenda vita ya kutumia ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutoa vitisho dhidi ya mataifa mengine na kueleza kwamba, hii ni mifano ya wazi ya ujeuri na ufidhuli wa utawala haramu wa Israel.
Baqaei amesema, kuna haja kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za maana kukabiliana na vitendo hivi vya utawala dhalimu wa Israel ambavyo vinakiuka waziwazi kanuni na sheria za kimataifa.