Magaidi wakamatwa kusini mashariki mwa Iran
Kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ametangaza kukamatwa asilimia 80 ya magaidi walioko kusini mashariki mwa Iran.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour, kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC), amezungumza kuhusu hali ya hivi karibuni mazoezi ya IRGC katika eneo la kusini mashariki, na kusema asilimia 80 ya magaidi katika eneo hilo wamekamatwa katika operesheni maalumu. Amesema katika operesheni hiyo iliyojumuisha pia ndege za kivita zisizo na rubani, vinara wakuu wa magaidi wameangamizwa.
Brigedia Jenerali Pakpour aidha ameeleza kuwa, baadhi ya magaidi wamejeruhiwa na wengine wametoroka na hivyo operesheni hiyo itaendelea hadi kukamatwa na kuuawa magaidi wote.
Kufuatia kushindwa utawala katili wa Kizayuni wa Israel katika mapambano na makundi ya muqawama na sanjari na uvamizi wa utawala huo uliolaaniwa dhidi ya baadhi ya maeneo ya Iran ya Kiislamu, mnamo Oktoba 26, magaidi wanaopata himaya ya utawala huo walitekeleza hujuma na kuua maafisa 10 wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wakilinda doria katika eneo la Taftan, mkoani Sistan na Mkoa wa Baluchistan, Kusini Mashariki mwa Iran.
Kufuatia shambulio hilo la kigaidi, vikosi vya IRGC vilianzisha operesheni ya kukabiliana na magaidi eneo hilo.