Satalaiti za kwanza za sekta binafsi Iran zatuma ishara za awali
Balozi wa Iran nchini Russia, Kazem Jalali, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: Ishara za kwanza za satalaiti mbili za "Kauthar na Hud-hud" zimepokewa kwenye kituo kilichoko ndani ya ardhi ya Iran, saa chache baada ya satalaiti hizo kuwekwa kwa ufanisi kwenye mzingo wa kilomita 500 wa dunia.
Katika mafanikio ya kihistoria kwa tasnia ya anga ya juu ya Iran jana Jumanne, sekta binafsi ya Jamhuri ya Kiislamu ilirusha kwa mafanikio satelaiti zake mbili za kwanza zilizotengenezwa na wataalamu wa Kiirani, Kauthar na Hud-hud, katika eneo la anga za mbali linalojulikana kama obiti kwa kutumia mtambo wa kurushia makombora yanayobeba satalaiti wa Soyuz nchini Russia.
Mafanikio haya yanaashiria uzinduzi wa sekta ya binafsi katika juhudi za uchunguzi wa anga za juu wa Iran.
Satalaiti mbili za "Kauthar" na "Hud-hud", zimeundwa na watafiti wa kituo cha binafsi cha "Omid Fezah Knowledge Base Company" zikiwa satalaiti za kwanza za sekta binafsi nchini Iran. Satalaiti hizi mbili zimetumwa kwa mafanikio kwenye mzingo wa anga za juu umbali wa kilomita 500 kutoka usawa wa bahari.
Satalaiti ya Kauthar, imeundwa kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na masuala ya kilimo, usimamizi wa maliasili, ufuatiliaji wa mazingira na kukabiliana na maafa.
Hud-hud, ni satelaiti ndogo ya mawasiliano iliyoundwa na sekta binafsi kwa ajili ya kuboresha mitandao ya mawasiliano inayotegemea satalaiti.
Matunda haya ni mwendelezo wa mafanikio ya sekta ya anga za juu ya Iran. Mapema mwaka huu, Jamhuri ya Kiislamu ilifanikiwa kurusha satalaiti ya utafiti ya Mahda kwa kutumia kombora la kurushia satalaiti la Simorgh (Phoenix) linalozalishwa nchini.