Rais wa Ghana awasili Iran
Rais John Dramani Mahama wa Ghana amewasili Tehran kwa ziara rasmi ambapo anatazamiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu nchini.
Akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kiuchumi na kisiasa, Rais Mahama aliwasili Tehran Jumamosi usiku kufuatia mwaliko wa mwenzake wa Iran Hassan Rouhani.
Rais wa Ghana alilakiwa katika Uwanja wa Ndege wa Mehrabad na Waziri wa Kilimo wa Iran Mahmoud Hujjati ambaye ni mwenyekiti wa upande wa Iran katika Tume ya Pamoja ya Iran na Ghana.
Rais Rouhani atamkaribisha rasmi Mahama leo Jumapili katika ikulu mjini Tehran.
Hii ni mara ya kwanza kwa rais wa Ghana kutitembelea Iran tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu miaka 37 iliyopita.
Rais Mahama anatazamiwa kukutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mbali na kufanya mazungumzo na Rais Rouhani pamoja na Spika wa Bunge Ali Larijani.
Siku ya Jumatatu atashiriki katika kikao cha pamoja cha kiuchumi na kibiashara cha wafanyabiashara na wajasrimali wa nchi mbili.
Akizungmza mapema Jumamosi na Shirika la IRIB, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran anayeshughulikia masuala ya Afrika Hossein Amir-Abdollahian amesema Iran inalipa umuhimu mkubwa suala la kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika.
Tokea yafikiwe mapatano ya nyuklia ya Iran na madola sita makubwa duniani mwezi Julai mwaka jana, viongozi wa ngazi za juu wa nchi kadhaa duniani wameitembelea Iran kwa lengo la kupanua uhusiani wa kibiashara, kiuchumi, kisisasa na kiutamaduni baina ya nchi zao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.