Baghaei: Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa hajakutana na Elon Musk
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baghaei amekanusha habari za kufanyika mkutano kati ya mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa na mshauri wa Rais mpya wa Marekani, Elon Musk.
Katika mahojiano yake na Shirika la Habari la Iran (IRNA) jana Jumamosi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baghaei alikanusha vikali madai yaliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani kuhusu kufanyika mkutano baina ya Elon Musk na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini New York, na kueleza kushangazwa kwake na madai hayo ya vyombo vya habari vya Marekani.
Gazeti la The New York Times limeripoti kuwa, mfanyabiashara bilionea wa Marekani, Elon Musk, ambaye alichangia pakubwa katika ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa hivi karibuni nchini humo, alikutana na mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeed Iravani, katika kikao cha siri mjini New York kujadili njia za kutuliza mvutano kati ya nchi hizo mbili.
Gazeti hilo limeongeza, likinukuu vyanzo viwili vya Iran ambavyo majina yao hayakutajwa kwamba: “Elon Musk, ambaye ni mshauri wa karibu wa rais mteule wa Marekani, Donald Trump, alikutana na mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Jumatatu iliyopita mjini New York na kufanya mazungumzo kuhusu kupunguza mivutano kati ya Iran na Marekani.”
Kwa mujibu wa vyanzo vya gazeti hilo, "mkutano huo ulifanyika katika eneo la siri na uliendelea kwa zaidi ya saa moja, na matokeo yake yalitathminiwa kuwa mazuri."