Iran yatoa wito kwa EU kubadili tabia ya ‘kiburi, kutowajibika’
(last modified Sat, 30 Nov 2024 02:48:34 GMT )
Nov 30, 2024 02:48 UTC
  • Iran yatoa wito kwa EU kubadili tabia ya ‘kiburi, kutowajibika’

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameutaka Umoja wa Ulaya kubadili tabia yake ya "kiburi na kutowajibika" mkabala wa Tehran huku mazungumzo kati ya wanadiplomasia wa Iran na Ulaya yakitarajiwa kuanza mjini Geneva.

Kazem Gharibabadi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya sheria na ya kimataifa amesena hayo akitoa maelezo kuhusu mkutano wa Alhamisi wa wajumbe wa Iran na Enrique Mora, Naibu Katibu Mkuu wa Huduma ya Nje ya Umoja wa Ulaya huko Geneva.

Ameandika kwenye mtandao wa X jana Ijumaa kwamba: "Ujumbe wa Iran, ulikuwa na majadiliano ya wazi na Mora kuhusu maswala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na masuala ya nyuklia na mazungumzo ya kuondoa vikwazo kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni."

"Ameelezwa tena kwamba EU inapaswa kuacha tabia yake ya ukiburi na kutowajibika kuhusu masuala na changamoto za kikanda na kimataifa," amesisitiza Gharibabadi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Ulaya haipaswi kuyahusisha matatizo na makosa yake yenyewe na wengine, ikiwa ni pamoja na kuhusu mzozo wa Ukraine."

Gharibabadi ameongeza kuwa, Ulaya "haina msingi wowote wa kimaadili" wa kufundisha wengine juu ya haki za binadamu kwa kuzingatia ushiriki wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani katika vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelea kufanywa na Israel huko Gaza, ambapo zaidi ya Wapalestina 44,300 wameuawa tangu Oktoba mwaka jana.