Israel yakiuka makubaliano ya kusitisha vita Lebanon, yaendelea kuua Wapalestina Ghaza
(last modified Fri, 29 Nov 2024 11:42:16 GMT )
Nov 29, 2024 11:42 UTC
  • Israel yakiuka makubaliano ya kusitisha vita Lebanon, yaendelea kuua Wapalestina Ghaza

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limefanya mashambulizi mapya dhidi ya Lebanon kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano liliyofikia na harakati ya Muqawama ya Hizbullah; na wakati huohuo limeshadidisha mashambulizi yake ya kinyama ya anga katika Ukanda wa Ghaza.

Taarifa iliyowekwa na jeshi la Lebanon kwenye mtandao wa X imesema, vikosi vya jeshi vamizi la Israel vimekiuka mara kadhaa makubaliano ya kusitisha mapigano baada tu ya kuanza kutekelezwa, na pia siku iliyofuata.
 
Taarifa hiyo imeongezea kwa kusema: "ukiukaji huu unajumuisha ukiukaji wa angani na mashambulizi katika ardhi ya Lebanon kwa kutumia silaha mbalimbali".
 
Jeshi la utawala ghasibu wa Israel limethibitisha kuwa lilifanya shambulio la anga jana Alhamisi kusini mwa Lebanon, na kuongeza kuwa vikosi vyake vimewafyatulia risasi pia watu waliokuwa wakiendesha magari kuelekea makwao katika eneo hilo.
 
Hapo awali vyombo vya habari vya Lebanon viliripoti kuwa watu wapatao wawili walijeruhiwa baada makombora ya vifaru vya jeshi la utawala wa Kizayuni kulenga miji mitano na baadhi ya mashamba ya kilimo kusini mwa nchi hiyo.
 
Mbunge wa Hizbullah Hassan Fadhlullah amesema: "adui Muisrael anawashambulia wale wanaorejea katika vijiji vya mpakani, leo kuna ukiukwaji uliofanywa na Israel hata katika hali hii."

Katika upande mwingine, jeshi la utawala haramu wa Israel limewaua shahidi Wapalestina wasiopungua 42 katika Ukanda wa Ghaza.

Ripoti zinasema askari wa jeshi la utawala huo wa Kizayuni wameshadidisha mashambulizi katika maeneo ya kati ya Ghaza na vifaru vya jeshi hilo vimesonga mbele zaidi katika eneo la kaskazini na kusini mwa ardhi hiyo ya Palestina.

Tangu Oktoba 2023 hadi sasa, jeshi la utawala haramu wa Israel limewaua shahidi Wapalestina wasiopungua 44,330 na kuwajeruhi wengine 104,933 katika vita vya kinyama na mauaji ya kimbari unayoendelea kufanya katika Ukanda wa Ghaza.../