Ombi la kukamatwa kiongozi wa kijeshi wa Myanmar
Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) amemshutumu kiongozi wa kijeshi wa Myanmar kwa kufanya jinai dhidi ya binadamu katika kuwakandamiza Waislamu walio wachache wa Rohingya.
Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai amesema kuwa atawasilisha ombi la kutolewa waranti ya kukamatwa Min Aung Hlaing kiongozi wa kijeshi wa Myanmar kwa kuhusika na jinai dhidi ya binadamu katika kukandamiza Waislamu walio wachache wa Rohingya.
Kwa kutilia maanani jinai nyingi zilizofanywa na watawala wenye misimamo ya kufurutu ada wa Myanmar katika kuwaua kwa umati Waislamu wa Rohingya, jamii ya kimataifa hususan wananchi wa Myanmar wamekuwa wakisubiri kesi ya watendajinai wa nchi hii kushughulikiwa haraka zaidi katika mahakama za kimataifa. Mbali na mauaji hayo ya halaiki, zaidi ya Waislamu milioni moja wa Rohingya wamelazimika kuhama makazi yao na kuishi katika hali mbaya zaidi kibinadamu katika nchi jirani kama vile Bangladesh kufuatia shambulio la kijeshi la jeshi la Myanmar lililoanza Agosti 2017.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wametaja jinai zinazofanywa na jeshi na Mabudha wenye itikadi kali dhidi ya Waislamu wa Rohingya kuwa ni mfano halisi wa mauaji ya kikabila. Kadiri kwamba watu wenye misimamo mikali wameteketeza moto mamia ya vijiji vya jimbo la Rakhine, magharibi mwa Myanmar, wakawatesa wakaazi na kufanya mauaji ya kinyama na ubakaji wa kimagenge kwa lengo la kuibua hofu na kuwafanya Waislamu wakimbie na kuacha nyuma mashamba na mali zao.
Ingawa serikali ya kijeshi ya Myanmar inakanusha tuhuma hizo, lakini kwa mujibu wa' tangazo la Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ombi la kukamatwa kwa mtawala wa kijeshi wa Myanmar limewasilishwa baada ya kufanyika uchunguzi wa kina, huru na usio na upendeleo, na maombi zaidi yako njiani kwa ajili ya kutolewa hati ya kukamatwa kwake kuhusiana na jinai hizo dhidi ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar.
Ingawa nchi hii si mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, lakini katika maamuzi ya 2018 na 2019, majaji walitangaza kwamba mahakama hiyo ilikuwa na mamlaka ya kufuatilia na kuchunguza jinai zilizofanyika nje ya mipaka ya nchi hiyo, na ambazo sehemu yake zilifanyika Bangladesh, mwanachama wa mahakama wa ICC, dhidi ya Waislamu wa Rohingya.
Kwa mujibu wa taarifa ya mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Jinai ICC, hili ni ombi la kwanza la kutolewa waranti ya kukamatwa kiongozi mkuu wa serikali ya Myanmar. Mahakama hiyo ya jinai imekuwa ikichunguza jinai hizo dhidi ya Waislamu wa Rohingya kwa takriban miaka mitano, na katika kuthibitisha hilo, imetumia ushahidi wa mashuhuda wakiwemo wa ndani ya Myanmar, nyaraka za kisayansi na ushahidi wa video.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ina nchi wanachama 124 na inategemea serikali husika kuwakamata washtakiwa. Kwa hiyo, kutokana na ukweli kwamba Min Aung Hlaing huwa hasafiri nje ya nchi, mahakama inakabiliwa na changamoto kubwa na kibarua kigumu cha kumkamata.
Ombi la Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai la kutolewa hati ya kukamatwa kiongozi wa kijeshi wa Myanmar limewasilishwa katika hali ambayo tayari waranti ya kukamatwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu mtendajinai wa utawala wa Israel na Yoav Gallant, waziri wa zamani wa vita wa utawala huo imetolewa kwa kuhusika kwao na jinai dhidi ya binadamu huko Gaza na Lebanon, jambo ambalo limekaribishwa na walimwengu na hivyo kufufua matumaini ya kuadhibiwa kisheria wahalifu hao wa vita.