Kiongozi Muadhamu: Hatima ya Israel ni kuondoka Asia Magharibi
(last modified Thu, 28 Nov 2024 13:38:44 GMT )
Nov 28, 2024 13:38 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Hatima ya Israel ni kuondoka Asia Magharibi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unaelekea kuondoka katika eneo la Asia Magharibi na kusisitiza kuwa, operesheni zinazoendelea za harakati za muqawama dhidi ya Israel haziwezi kusitishwa.

Ujumbe ulioandikwa katika akaunti rasmi ya Ayatullah Khamenei ya lugha ya Kiajemi kwenye jukwaa la X inasomeka hivi: "Kimbunga cha Al-Aqsa hakiwezi kuzimwa, na utawala ghasibu wa Kizayuni unaelekea kuondoka."

Ujumbe huo ambao umenukulu kauli ya Kiongozi Muadhamu umeandamana na mchoro wa Kifaru cha utawala wa Kizayuni wa Israel ambacho kinaelekea kumezwa na ardhi huku bendera nyeupe ikiinuka katika mtutu wake.

Harakati za muqawama, zikiwemo Hamas na Jihad Islami katika Ukanda wa Gaza na Hizbullah ya Lebanon na hali kadhalika harakati za muqawama huko Iraq na Yemen, zilianzisha operesheni hiyo ya Kimbunga cha Al Aqsa Oktoba mwaka jana baada ya utawala wa Kizayuni kuanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza.