Naim Qassim: Muqawama wa wanamapambano wa Kiislamu umeishangaza dunia
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, wanamapambano wa kambi ya Muqawama wako tayari kuendelea kupambana na adui wakati wowote watakapolazimika kufanya hivyo.
Sheikh Naim Qassem amesema hayo alfajiri ya leo Jumamosi ikiwa ni hotuba yake ya kwanza kabisa tangu kuanza utekelezaji wa makubaliano ya kusimamisha vita baina ya Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sehemu ya kwanza kabisa ya hotuba ya Katibu Mkuu wa Hizbullah imewalenga wananchi wa Lebanon hususan wa kusini mwa nchi hiyo na kuwapongeza kwa subira ya kupigiwa mfano waliyoionesha, kwa Jihadi yao, kwa kuvumilia kuondoka kwenye maeneo yao na kuhamia maeneo mengine na kwa jinsi vijana wa maeneo hayo walivyosimama imara kukabiliana na adui. Amewaahidi wananchi hao kuwa wana wao wataendelea kuwa imara kwenye medani ya mapambano.
Vilevile amesema kuwa, utawala wa Kizayuni umeendesha vita vya siku 64 kwa shabaha ya kuingamiza Hizbullah, kuwafanya wakimbizi wananchi wa Lebanon na kujaribu kutekeleza njozi yake ya kuunda Mashariki ya Kati Kubwa lakini umeshindwa kikamilifu kwani Hizbullah ilishambulia ndani kabisa ya ardhi za Palestina zinazokaliwa yanayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni zilizopachikwa jina bandia la Israel na kumlazimisha adui kuingia kwenye hali ya kujilinda na si kushambulia.
Amesema, katika vita hivyo, walowezi 70,000 wa Kizayuni wamekuwa wakimbizi na Muqawama umeonesha jinsi ulivyojiandaa vilivyo kukabiliana na adui kiasi kwamba Muqawama wa wanamapambano wa Kiislamu umeishangaza dunia na kulitia kiwewe jeshi la Israel.