Tarehe ya mazishi ya Mashahidi Nasrallah na Safieddine kutangazwa hivi karibuni
Tarehe ya mazishi ya hayati kiongozi wa Hizbullah Shahidi Sayed Hassan Nasrallah na pia kiongozi mwingine wa harakati hiyo ya muqawama Shahidi Sayyid Hashem Safieddine itatangazwa hivi karibuni.
Taarifa kuhusu mpango wa mazishi ya Sayyid Nasrallah imetangazwa na Ibrahim al-Musawi ambaye amesema hayo baada ya kutangazwa kusitishwa mapigano kati ya Hizbullah na utawala ghasibu wa Israel.
Ameyapongeza makundi yote ya Lebanon kwa makubaliano ya usitishaji vita na kusisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umelazimika kukubaliana nao baada ya kushindwa kufikia malengo uliyojiwekea wenyewe kwa ajili ya vita dhidi ya Lebanon.
Utawala wa Israel ulijaribu kukandamiza harakati ya Hizbullah lakini ulishindwa kufanya hivyo na kulazimika kukubaliana na mapatano hayo, amesema.
Al-Musawi ameongeza kuwa mazungumzo juu ya usitishaji vita yalifanyika kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kwamba Hizbullah inasisitiza kutekelezwa kwa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Amendelea kusema kuwa kutatangazwa muda na mahali mwafaka kwa ajili ya mazishi ya kiongozi huyo aliyeuawa shahidi wa Hizbullah katika siku za usoni.
Wakati huo huo Mahmoud Qamati, naibu mkuu wa Baraza la Kisiasa la Hizbullah amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa pia kuna mpango wa mazishi ya Shahidi Sayyid Hashem Safieddine, kiongozi mwandamizi wa Hizbullah ambaye naye pia aliuawa shahidi katika hujuma ya utawala haramu wa Israel.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon yalianza kutekelezwa Jumatano alfajiri, na kuibua matumaini baada ya miezi 14 ya vita.
Sayyed Hassan Nasrallah, ambaye aliongoza Hizbullah kwa zaidi ya miaka 32, aliuawa shahidi katika shambulio kubwa la anga ambalo Israel ililitekeleza kusini mwa Beirut mnamo Septemba 27 kwa kutumia mabomu ya kivita ya Marekani.
Aliteuliwa kuwa mkuu wa Hizbullah mwaka 1992 baada ya kuuawa shahidi kwa aliyekuwa katibu mkuu wakati huo Abbas al-Musawi.