Hamas: Kusitisha mapigano na Hizbullah kumesambaratisha ndoto ya Israel
(last modified Thu, 28 Nov 2024 07:14:32 GMT )
Nov 28, 2024 07:14 UTC
  • Hamas: Kusitisha mapigano na Hizbullah kumesambaratisha ndoto ya Israel

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imesema hatua ya utawala haramu wa Israel ya kukubali kusitisha vita na Hizbullah ni dalili ya kusambaratika ndoto potofu ya Waziri Mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu ya kutumia nguvu za kijeshi kubadilisha muundo wa Asia Magharibi.

Siku ya Jumanne, Netanyahu alilazimika kukubali mapatano ya usitishaji vita baada ya mashambulizi ya miezi 14 dhidi ya Lebanon. Hizbullah imekuwa ikijibu vikali mashambulizi hayo na kuisababishia Israel hasara kubwa.

Hamas imesema katika taarifa kwamba: "Kukubali adui makubaliano na Lebanon bila kutimiza masharti aliyoweka ni hatua muhimu katika kusambaratisha ndoto potofu za Netanyahu za kubadilisha ramani ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibu) kwa nguvu."

Hamas imesema ndoto ya Netanyahu ya kuishinda Hizbullah na kuipokonya silaha pia imesambaratika.

Utawala wa Israel umeua zaidi ya watu 3,700 nchini Lebanon, wakiwemo mamia ya wanawake na watoto na kuwajeruhi wengine karibu 15,700 tangu Oktoba mwaka jana.

Wakati huo hyuo Hizbullah imesisitiza kuwa iko tayari kabisa kukabiliana na hujuma yoyote tarajiwa ya Israel dhidi ya Lebanon. Katika taarifa Jumatano, Harakati ya Muqawama ya Hizbullah imesema Israel imekubali usitisaji vita kutokana na maelfu ya operesheni zilizofanikiwa za harakati hiyo.