Iran yalaani kuendelea mashambulizi ya Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani mashambulizi mapya ya anga ya Marekani na Uingereza kwenye miundombinu ya mkoa wa Sa'ada wa kaskazini mwa Yemen.
Esmail Baghaei Hamaneh amesema hayo leo na kutoa mwito wa kukomeshwa mara moja mashambulizi ya kijinai ya Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Yemen.
Amesema huo ni ukiukaji wa wazi wa haki ya kujitawala ardhi ya Yemen na ni kukanyaga sheria za kimataifa ikiwemo hati iliyounda Umoja wa Mataifa.
Vilevile ameonya kwamba mashambulizi hayo ya Marekani, Uingereza na Israel dhidi ya Yemen yatazidi kuhatarisha usalama na kusababisha ukosefu wa utulivu katika eneo la Asia Magharibi.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha amegusia jinai na kuendelea mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na kulaani uungaji mkono wa kijeshi na kisiasa wa Marekani na Uingereza kwa utawala wa Kizayuni.
Amesema kuwa, uungaji mkono huo ni sawa na kushiriki moja kwa moja katika jinai za kutisha za kivita wanazofanyiwa wananchi madhlumu wa Palestina hawa wa Ukanda wa Ghaza.
Aidha Baghaei Hamaneh amepongeza nafasi adhimu ya wananchi wa Yemen na mataifa mengine huru katika mshikamano na uungaji mkono kwa wananchi wa Palestina na kutoa mwito wa kuchukuliwa hatua za dhati zaidi na jamii ya kimataifa na nchi za Kiislamu hususan kupitia jumuiya ya OIC, ili kukomesha mara moja mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.