Salami: Mhimili wa Muqawama upo katika 'kilele cha nguvu zake"
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) amesema kuwa Mhimili wa Muqawama katika eneo la Magharibi mwa Asia upo katika kilele cha nguvu zake.
Meja Jenerali Hossein Salami amesema Mhimili wa Muqawama upo katika kilele cha uwezo na nguvu zake hata hivyo maadui wamegeuka wenzo wa kueneza chuki wakiwa wamejawa woga. Kamanda Salami ameeleza haya leo katika mji wa Kerman, kusini mashariki mwa Iran.
Ameipongeza harakati ya Hizbullah ya Lebanon kwa kuwa ngangari mkabala wa Israel na kuashiria oparesheni za kulipiza kisasi za harakati hiyo zilizoilazimisha Tel Aviv ikubali masharti ya kusitisha vita na hivyo kufikiwa mapatano yaliyohitimisha mashambulizi ya Israel huko Lebanon.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) ameeleza kuwa, kuendelea kuwepo harakati ya Hizbullah katika mkondo wake licha ya hatari zote nzito kunatokana na mapambano yaliyoongozwa na Katibu Mkuu wake wa zamani, Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na afisa wa ngazi ya juu wa harakati hiyo Shahidi Hashim Safiyuddin ambao walifanikiwa kupanda mizizi ya jihad na mapambano ndani ya imani ya vijana wa Lebanon.
Kamanda Salami ambaye amehudhuria hafla ya kumuezi Shahidi Jenerali Qassim Soleimani aliyeongoza vita dhidi ya ugaidi katika eneo la Asia Magharibi, amempongeza pia Shahidi Soleimani kwa kujitolea kwake kwa ajili ya mataifa ya Kiislamu ambapo aliongoza mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi ya Takfiri yanayoungwa mkono na kusaidiwa na nchi za Magharibi na utawala wa Israel.