Zarif: Iran sio tishio la usalama kwa nchi yoyote ile
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i121784-zarif_iran_sio_tishio_la_usalama_kwa_nchi_yoyote_ile
Makamu wa Rais katika Masuala ya Kistratejia wa Iran, Mohammad Javad Zarif amesema Jamhuri ya Kiislamu si tishio la usalama kwa nchi yoyote ile duniani, akisisitiza kwamba kama Tehran ingelikusudia kutengeneza silaha za nyuklia, ingelikuwa imefanya hivyo zamani.
(last modified 2025-01-23T04:07:18+00:00 )
Jan 23, 2025 04:07 UTC
  • Zarif: Iran sio tishio la usalama kwa nchi yoyote ile

Makamu wa Rais katika Masuala ya Kistratejia wa Iran, Mohammad Javad Zarif amesema Jamhuri ya Kiislamu si tishio la usalama kwa nchi yoyote ile duniani, akisisitiza kwamba kama Tehran ingelikusudia kutengeneza silaha za nyuklia, ingelikuwa imefanya hivyo zamani.

Zarif amesema hayo katika mahojiano na mtangazaji wa kipindi cha GPS cha CNN, Fareed Zakaria, pambizoni mwa mkutano wa kila mwaka wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) huko Davos, Uswisi.

Ameeleza bayana kuwa, "Iran sio tishio la usalama. Baadhi wanajaribu kuiarifisha Iran kama tishio la usalama na kutumia chuki dhidi ya Iran (Iranophobia) na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) kuhalalisha matendo yao dhidi ya watu wasio na hatia, ikiwa ni pamoja na Gaza. Hata hivyo, madai haya hayana msingi wowoye.” 

Dakta Zarif ambaye aliongoza mazungumzo ya nyuklia na madola yenye nguvu duniani ambayo kilele chake ni kufikiwa mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015, amesema wale wanaodai kuwa Iran ipo mbioni kutengeneza bomu la nyuklia, walipaswa kukumbatia Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ambao uliundwa kwa ajili ya kutekeleza mpango wa nyuklia wa Iran na kuzuia eti Iran kupata silaha za nyuklia kwa angalau miaka 15.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa, "Iran daima imekuwa tayari kwa mazungumzo na ushirikiano na nchi za kikanda. Pendekezo letu la kuanzisha utaratibu wa mazungumzo ya kikanda unaoitwa 'Jukwaa la Mazungumzo la Asia Magharibi' linaonyesha dhamira yetu ya amani na utulivu katika eneo hili." 

Akiashiria maonyo ya muda mrefu ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu juu ya Iran eti kuzalisha silaha ya nyuklia ndani ya miezi sita, Zarif alisema kuwa karibu miaka 30 imepita tangu madai hayo yatolewe, lakini Iran inaendelea kudaiwa kuwa ni tishio lililo karibu.