Pezeshkian awataka Wairani kuwa macho mkabala wa njama za maadui
Rais wa Iran amesisitiza haja ya kudumisha umoja wa kitaifa nchini, wakati huu ambapo maadui wa taifa hili wanakula njama na kutaka kutumia vibaya mizozo ya ndani.
Akizungumza katika mkutano na wanaharakati wa kisiasa, kijamii na kiutamaduni katika mji wa Ahvaz, mkoa wa Khuzestan, kusini-magharibi mwa nchi Jumatano jioni, Rais Masoud Pezeshkian amewataka wananchi wa Iran kuimarisha umoja na kushikana mikono kujenga nchi yao ili kuwakatisha tamaa maadui wanaotaka kutumia vibaya mizozo ya ndani nchini Iran.
Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa: "Tunapaswa kushikamana na kuijenga Iran kwa umoja na mshikamano ili kuwakatisha tamaa maadui."
Pezeshkian amesema kuwa mivutano na utesi ndio chanzo cha matatizo mengi na ukosefu wa mafanikio nchini na kuongeza kuwa, wananchi wanapaswa kujua kuwa, mafanikio yanapatikana kwa ushirikiano na huruma.
Rais ameonya kwamba, ikiwa matatizo yatabaki bila kutatuliwa, "maadui watatumia kila fursa kutudhuru", na wataweza kulinda maslahi yao wenyewe kutokana na migawanyiko hapa nchini.
"Haya ndiyo matokeo pekee yanayotokana na mizozo ya ndani na ukosefu wa huruma," Pezeshkian ameongeza huku akionya kwamba, hili ni tishio kubwa linalohatarisha "utambulisho wetu wa kijamii na kiutamaduni" na mambo yote ambayo yanaimarisha mshikamano nchini kote.