Spika wa Baraza la Hamas apongeza mchango wa Iran katika kuwatetea Wapalestina
Muhammad Ismail Darwish, Mwenyekiti wa Shura ya Hamas, ametoa shukurani kwa msaada na uungaji mkono wa Iran kwa watu wa Palestina, na kusema mchango wa Tehran ni muhimu katika mapambano yanayoendelea dhidi ya utawala wa ghasibu wa Israel.
Muhammad Ismail Darwish ametoa shukrani hizo katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi, mjini Doha, Qatar.
Ismail Darwish ameeleza kuwa, Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ilikuwa semehu muhimu katika njia ya mapambano ya watu wa Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa, mipango na matarajio ya utawala huo ya kuwatenganisha wananchi wa Palestina na ardhi yao kwa kuanzisha vita vya mauaji ya kimbari na kadhalika haitakuwa na tija.
Mkuu wa Shura ya Hamas pia ameongeza kuwa: "Watu wa Palestina wamekita mizizi katika ardhi yao na wanashikamana na haki zao, maeneo matakatifu na Msikiti wa Al-Aqsa."
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesisitiza uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu kwa mapambano ya wananchi wa Palestina na kusema: Muqawama wa kishujaa wa watu wa Ukanda wa Gaza umeuthibitishia ulimwengu uwongo wa kutoshindwa jeshi la Israel.
Sayyid Abbas Araqchi amesema: "Watu wa Ukanda wa Gaza waliweza kutekeleza operesheni ya kishujaa isiyo na kifani katika uwanja wa mapambano na mazungumzo ya kiwango cha juu yaliyopelekea kusitishwa mapigano na mapatano ya heshima ya kubadilishana mateka."