Kiongozi Muadhamu amteua Naim Qassem kuwa mwakilishi wake Lebanon
(last modified Wed, 05 Feb 2025 12:29:44 GMT )
Feb 05, 2025 12:29 UTC
  • Kiongozi Muadhamu amteua Naim Qassem kuwa mwakilishi wake Lebanon

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, katika dikrii, amemuarifisha Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawamaya ya Hizbullah, Sheikh Naim Qassem kama mwakilishi wake nchini Lebanon.

Baada ya kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na utawala katili wa Israel, Sheikh Naim Qassem aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon.

Hapo awali, Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah ndiye aliyekuwa mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Iran nchini Lebanon. 

Kuteuliwa kwa Sheikh Naim Qassem kuwa mwakilishi wa Imam Khamenei nchini Lebanon kunatuma ujumbe muhimu kuhusu mustakabali wa Muqawama wa Lebanon na Asia Magharibi, kufuatia vita vya Israel vilivyoanza tarehe 7 Oktoba 2023.

Sheikh Naim Qassem aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah, baada ya kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah 

Katika hatua nyingine, Hizbullah imelaani vikali hatua ya Australia ya kumuwekea vikwazo Katibu Mkuu wa harakati hiyo Sheikh Naim Qassem, ikisema kwamba hatua hiyo inathibitisha Canberra inatumiwa kama chombo cha kuendeleza ajenda ya Marekani na utawala wa Kizayuni.

"Uamuzi huu usio wa haki hauna msingi wa kisheria au wa kimaadili, lakini unaashiria upendeleo wa wazi kwa kundi la Kizayuni na unatumika kuficha jinai, uvamizi na ugaidi," harakati hiyo imesema, ikirejelea mauaji ya halaiki huko Gaza.

Hatua hiyo dhidi ya Sheikh Qassem ilitangazwa Jumatatu na Wizara ya Mambo ya Nje ya Australia kwa madai yasiyo na msingi kwamba mwanachuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu "anafadhili ugaidi."