Iran yaonesha sehemu ya nguvu zake za makombora mapya
Mfumo wa kimkakati wa ulinzi wa anga wa masafa marefu wa Bavar 373 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umepasi katika majaribio kwa kutungua kwa umahiri vyombo vilivyokuwa vinaruka katika masafa ya juu angani. Hayo yamefanyika kwenye mazoezi ya kijeshi ya anga ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaliyopewa jina la Eqtedar 1403.
Majaribio hayo ya mfumo wa kimkakati wa kujilinda na mashambulizi ya anga uitwao Bavar 373 yamefanyika mwishoni mwa awamu ya pili ya luteka ya ulinzi wa anga ya Eqtedar 1403. Bavar 373 ni mfumo wa kiistratejia wa ulinzi wa anga wa masafa marefu ambao umebuniwa na kutengenezwa na wataalamu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Wakati unafanyiwa majaribio, mfumo huo wa ulinzi ambao siri yake hakuna anayeijua ila Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yenyewe, umefanikiwa kutungua shabaha hasimu kwa umahiri wa hali ya juu.
Katika sehemu hiyo ya mazoezi ya kijeshi ya Iran, ndege za 'adui' zilitumwa kufanya shambulio la kimazoezi jangwani, katikati mwa Iran bila ya kutangazwa, lakini mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya anga wa Bavar 373 ulikuwa makini kugundua ndege hizo na kufanikiwa kuzitungua kabla ya kufanya shambulio lolote.
Kuwepo kwa wakati mmoja mifumo ya ulinzi wa anga ya S-300 na Bavar 373 na ushirikiano katika uendeshaji wa mifumo hiyo kwa wakati mmoja ni kati ya mambo muhimu yaliyokuwemo kwenye luteka hiyo ya kijeshi ya karibuni zaidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.