Pezeshkian: ECO ni jukwaa muhimu la ushirikiano baina ya nchi za Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i122380-pezeshkian_eco_ni_jukwaa_muhimu_la_ushirikiano_baina_ya_nchi_za_kiislamu
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametilia mkazo wajibu wa kustawishwa uhusiano kati ya nchi za Kiislamu na amesema: "Jumuiya ya ECO inaweza kuwa jukwaa linalofaa mno kwa ajili ya kuleta maelewano na ushirikiano kati ya mataifa ya Kiislamu."
(last modified 2025-02-06T03:26:21+00:00 )
Feb 06, 2025 03:26 UTC
  • Pezeshkian: ECO ni jukwaa muhimu la ushirikiano baina ya nchi za Kiislamu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametilia mkazo wajibu wa kustawishwa uhusiano kati ya nchi za Kiislamu na amesema: "Jumuiya ya ECO inaweza kuwa jukwaa linalofaa mno kwa ajili ya kuleta maelewano na ushirikiano kati ya mataifa ya Kiislamu."

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi (ECO) ni jumuiya ya kikanda ya kiserikali iliyoanzishwa mwaka 1985 na nchi za Kiislamu za Iran, Pakistan na Uturuki. Mwaka 1992, jumuiya hiyo ilipokea wanachama wapya saba yaani nchi za Afghanistan, Azerbaijan, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Turkmenistan na Uzbekistan.

Eneo linalojumuisha nchi za ECO lina fursa nyingi za kibiashara na lina nafasi muhimu kimataifa, lakini pamoja na hayo ECO inakumbana na changamoto nyingi katika kufikia malengo yake.

Rais Masoud Pezzekian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema jana jioni (Jumatano) wakati alipoonana na Asad Majid Khan, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi (ECO) kwamba, jumuiya hiyo inaweza kuwa jukwaa bora la kuleta maelewano na ushirikiano kati ya nchi za Kiislamu lakini kwa bahati mbaya tunaona jumuiya hiyo inashindwa kufikia malengo yake.

Aidha amemtakia mafanikio Katibu Mkuu mpya wa ECO. Amesema: "Ninatumai kuwa kwa mipango mipya na katika mikutano ya siku zijazo, tutashuhudia kufufuliwa ushirikiano na maingiliano mapya kati ya wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa ECO."

Katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu mpya wa jumuiya ya ECO, Asad Majid Khan amesisitizia nafasi muhimu ya Iran katika jumuiya hiyo na kusema: "Ninatumai kwamba katika kipindi changu cha uongozi kwenye nafasi hii, tutaweza kushuhudia mabadiliko na ufufuaji wa uwezo wa ECO."