Mwangwi wa maandamano ya Bahman 22 katika vyombo vya habari vya Marekani
Vyombo vya habari vya lugha ya Kiingereza vimeyapa kipaumbele maalumu maadhimisho ya miaka 46 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yaliyofanyika jana kote nchini.
Shirika la habari la Associated Press limesema katika ripoti yake kuhusu mwaka wa 46 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba sherehe hizo zimefanyika kwa mara ya kwanza tangu Donald Trump arejee Ikulu ya White House na kuanza tena kampeni ya "mashinikizo ya juu zaidi" dhidi ya Iran, na kwamba "makumi ya maelfu ya Wairani" walimiminika mabarabarani katika hali ya baridi kali iliyofikia nyuzi joto chini ya sifuri.
Shirika hilo la habari la Marekani limeandika kuwa, Iran inakabiliwa na vikwazo vikali, na kwamba vitisho vya Trump vya kuzidisha vikwazo hivyo vimetolewa huku akitangaza kuwa anataka kufikia makubaliano na Tehran kuhusu miradi yake ya nyuklia inayoendelea kustawi.
Ripoti ya Associated Press inaendelea kusema: "Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, alisema Ijumaa iliyopita (Februari 7) kwamba "hakupaswi kufanyika mazungumzo na serikali ya aina hiyo." Hata hivyo, hakukataza waziwazi kuamiliana na Washington."
Mjini Tehran, maelfu ya watu waliandamana kuelekea Azadi Square licha baridi kali, wakiwa wameshikilia bendera, puto na mabango yenye nara na kaulimbiu za kimapinduzi. Waandamanaji hao walitoa nara za "Mauti kwa Marekani" na "Mauti kwa Israel" huku wakiwa wamebeba picha za Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, na bendera za Iran, Palestina, Hizbullah na Hamas.
Vikosi vya jeshi la Iran pia vilionyesha mifano ya baadhi ya makombora yao.