Iran yataka kuimarishwa ushirikiano wa kiuchumi wa "D-8"
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran anayeshughulikia diplomasia ya uchumi amesisitiza utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya wanachama wa Jumuiya ya Nchi Nane Zinazostawi za Kiislamu (D-8).
Sayyid Rasoul Mohajer, ameyasema hayo katika mazunguumzo yake na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi Nane Zinazostawi za Kiislamu (D-8), akieleza utayarifu wa Iran kuendelea kuunga mkono jumuiya hiyo. Vilevile amewasilisha mapendekezo kwa Katibu Mkuu wa D-8 kwa ajili ya kupanua ushirikiano katika maeneo kama vile biashara, forodha, bidhaa za kilimo, biashara ndogo ndogo na za kati, utalii na utalii tiba na huduma za visa.
Kwa upande wake, Isiaka Abdulqadir Imam, Katibu Mkuu wa D-8 pia amewasilisha ripoti juu ya programu za hivi karibuni za jumuiya hiyo. Amepongeza mchango athirifu wa Iran katika kupeleka mbele malengo ya D-8 na kusema: Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa mwanachama mwenye taathira wa Jumuiya ya Nchi Nane Zinazostawi za Kiislamu na kwa sasa ni mwenyeji wa taasisi mbili amilifu za D-8, ambazo ni Taasisi ya Sayansi na Teknolojia na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha jumuiya hiyo ambacho kiko Hamedan.
Nchi nane zinazostawi aa Kiislamu ni Iran, Uturuki, Pakistan, Misri, Nigeria, Bangladesh, Malaysia na Indonesia. Katika mkutano wa hivi karibuni wa wakuu wa nchi hizo mjini Cairo, Jamhuri ya Azerbaijan ilikubaliwa kuwa mwanachama wa tisa wa D-8.