Kamanda Pourdastan: Iran itaimarisha uwezo wake wa kiulinzi sambamba na vitisho
Kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran amesema kuwa vikosi vya ulinzi vya nchi hii vimejitolea kukuza uwezo wa kiulinzi kulingana na vitisho vinavyoibuka dhidi ya taifa.
Brigedia Jenerali Ahmad Reza Pourdastan ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Kistratejia cha Jeshi la Iran ametilia mkazo umuhimu wa ubunifu katika tasnia ya ulinzi.
"Ni lazima tuzidishe uwezo wa kufanya utafiti ili kupiga hatua katika uwezo wa kiulinzi", amesema Kamanda Ahmad Reza Pourdastan.
Kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran amesema mabeberu wa kimataifa wamemeanzisha vita mseto kwa kutumia kwa wakati mmoja nguvu zao zote kutoa pigo kwa nchi lengwa.
Brigedia Jenerali Pourdastan ameashiria vitisho vya Rais Donald Trump dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa Trump na washirika wake wanataka kuibua vita, hivyo inapasa kujiandaa kukabiliana na vitisho vya adui.
Amesema, jeshi la Iran si tu linahusika na masuala ya kijeshi bali linaweza kutoa mchango katika sekta za ujenzi, misaada na utoaji huduma.