Araqchi: Silaha za nyuklia za Israel ni tishio na hatari kwa dunia
Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa jamii ya kimataifa inapasa kuushinikiza utawala wa Israel kujiunga na Mkataba Unaozuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) ili shughuli zake za nyuklia ziwe chini ya usimamizi na ukaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA).
Araqchi ameeleza haya jana Jumatatu katika hotuba aliyoitoa kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi Kuhusu Upokonyaji Silaha.
Ameongeza kuwa, silaha za maangamizi ya halaiki zikiwemo za nyuklia zinazomilikiwa na utawala ghasibu wa Israel ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa utawala wa Israel unakwamisha kuwepo kwa eneo pasina silaha za nyuklia katika eneo la Asia Magharibi na unaendelea kuzitishia nchi nyingine kwa silaha za nyuklia.
Utawala wa Kizayuni unakadiriwa kumiliki vichwa vya nyuklia kuanzia 200 hadi 400.
Utawala wa Kizayuni wa Israel ndio pekee ambao si mwanachama wa NPT katika eneo la Asia Magharibi licha ya kujilimbikizia silaha hatari za mauaji ya halaiki.
Araqchi ameongeza kuwa, utawala ghasibu wa Israel una rekodi ya kutisha zaidi ya uvamizi na ukaliaji mabavu, kutekeleza mauaji ya kimbari, jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu katika karne ya 21 katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu; hatua ambazo haziwezi kuvumiliwa na dhamiri ya mwanadamu.