Pezeshkian: Iran imeazimia kuimarisha ushirikiano na Russia
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian ameahidi kunyanyua kiwango cha uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Russia kwa kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya pande mbili, na kuimarisha maingiliano athirifu katika masuala ya kikanda.
Katika mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov aliyeko safarini hapa Tehran, Pezeshkian ameeleza kuwa, uhusiano wa pande mbili unakua na kusisitiza haja ya kuharakisha utekelezaji wa makubaliano, haswa makubaliano ya kimkakati na ya kina kati ya nchi hizi mbili.
Rais Pezeshkian ameeleza bayana kuwa, "Iran na Russia zina uwezo mkubwa wa kuimarisha ushirikiano wao, na tumeazimia kuimarisha maingiliano kati ya Tehran na Moscow."
Aidha amesisitiza umuhimu wa kuwa na ushirikiano endelevu na wenye kujenga kati ya mataifa hayo mawili.
"Iran na Russia zina mitazamo inayowiana kwa karibu kuhusu masuala ya kikanda, na zinataka kuimarisha ushirikiano wao wa kikanda na kimataifa, kupitia maingiliano ya pande mbili na kupitia mashirika kama vile Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, Jumuiya ya Eurasia na BRICS," Rais amesema.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia pia amesisitiza kwamba, juhudi zote zitafanywa kwa shabaha ya kuimarisha ushirikiano unaostawi, na kutekeleza makubaliano ya pande mbili, haswa makubaliano ya kistratajia baina pande mbili.
Lavrov amesema kukamilika mchakato wa Iran kujiunga na Jumuiya ya Kiuchumi ya Eurasia kutatoa njia mpya na madhubuti ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili, haswa katika nyanja za kiuchumi na kibiashara.
"Iran na Russia zina maslahi mengi ya pande mbili katika kudumisha ushirikiano wa kieneo wenye ufanisi," amesema mwanadioplomasia huyo mkuu wa Russia.