Mkuu wa IRGC: Maadui wa Iran bado hawajapata vipigo 'vikali'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i123244-mkuu_wa_irgc_maadui_wa_iran_bado_hawajapata_vipigo_'vikali'
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amepongeza uwezo wa kiulinzi na kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa, maadui wa Iran bado hawajapata vipigo 'vikali' licha ya mashambulizi na operesheni kadhaa za kulipiza kisasi zilizofanywa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
(last modified 2025-02-26T10:07:30+00:00 )
Feb 26, 2025 10:07 UTC
  • Mkuu wa IRGC: Maadui wa Iran bado hawajapata vipigo 'vikali'

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amepongeza uwezo wa kiulinzi na kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa, maadui wa Iran bado hawajapata vipigo 'vikali' licha ya mashambulizi na operesheni kadhaa za kulipiza kisasi zilizofanywa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Meja Jenerali Hossein Salami ameyasema hayo leo alipokuwa akihutubia vitengo vya IRGC na vikosi vya wapiganaji wa kujitolea vya Basij vilivyoshiriki katika mazoezi ya pamoja ya kijeshi yaliyopewa jina la Payambar-e-A’azam (Mtume Aadham) 19 yaliyofanyika katika Mkoa wa Markazi.
 
Jenerali Salami ameeleza kwamba, nguvu halisi za Iran zinaweza kuitikisa dunia, na akaongeza kuwa maadui inapasa wajihadhari na vipigo ilivyotoa Iran kama vile vya Operesheni za Ahadi ya Kweli 1 na 2, zilizotekelezwa mwaka jana dhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni yaliyopachikwa jina bandia la Israel.
 
"Iran ni nafsi moja na yenye nguvu na inaweza kuitikisa dunia. Iran ni kubwa na maadui bado hawajapata vipigo vikali vya Iran, na kila walichokiona hadi sasa katika operesheni za Ahadi ya Kweli kilikuwa ni onyo na mfano tu,” amesisitiza mkuu huyo wa IRGC.
 
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kuwa, ikiwa maadui hawajifunzi kutokana na historia ya Jamhuri ya Kiislamu ya miaka 46 na wakaendeleza uovu wao, itapasa watarajie kupata fedheha na idhilali ambayo wameipata katika miaka 46 iliyopita wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kusonga mbele.
 
Sambamba na kusisitiza kwamba Iran imekuwa imara zaidi kwa miaka kadhaa sasa na inajitegemea na ina nguvu, Jenerali Salami amesema, Jamhuri ya Kiislamu inafuata njia ya fikra ambayo haiwezi kufutwa na maadui na kwamba misamiati kama mapambano, kujitawala na uhuru ni miongoni mwa malengo yake matukufu inayoshikamana nayo daima dawamu.

Kamanda wa IRGC amebainisha kuwa, Marekani na Israel zilipanga njama za kuwatenga kisiasa watu wa Iran na kujaribu kutikisa mioyo ya mataifa, hususan taifa la Iran kwa operesheni kali za kisaikolojia, lakini wamefeli katika kila njama waliyobuni.

Aidha amesisitiza kuwa Washington na Tel Aviv hazikuweza kuushinda Ukanda wa Ghaza na Muqawama wa Palestina katika eneo hilo lililowekewa mzingiro.../