Tehran yajibu matamshi ya Uturuki dhidi ya Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan dhidi ya sera za kieneo za Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa, nchi hii haibadilishi sera zake kila siku.
Esmaeil Baghaei amethibitisha kujitolea kwa Iran kufungamana na "misimamo yake ya msingi," akisisitiza kwamba nchi hii haibadilishi sera zake siku baada ya siku.
Baghaei amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) jana Ijumaa na kuongeza kwamba, “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikiunga mkono Muqawama huku ikikabiliana kwa dhati na mienendo haramu ya ugaidi.”
Pia amesisitiza kuwepo Iran katika mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugaidi. "Tulikuwa nchi ya kwanza kupandisha bendera ya mapambano dhidi ya Daesh (kundi la kigaidi na kitakfiri) na misimamo mikali ya kufurutu ada kwa mikono ya shujaa wetu wa taifa, Shahidi (Kamanda wa kupambana na ugaidi Jenerali Qassem) Soleimani, na tukawashinda katika eneo hili."
Baghaei ameashiria kukataa mapema kwa Tehran jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya Uturuki na kusema, "Tulikuwa nchi ya kwanza kupinga na kukabiliana na mapinduzi dhidi ya serikali ya Uturuki. Tulikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kukaribisha upokonyaji wa silaha wa wapiganaji wa Kikurdi (PKK), na kuiona kuwa hatua muhimu kuelekea kuimarisha usalama katika nchi jirani ya Uturuki.
Kadhalika Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amemnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan akisema, "Eneo hili lazima liwe huru kutoka kwa utamaduni wa nchi moja kutawala nyingine; si Waarabu, wala Waturuki, wala Wakurdi, wala Wairani, (wote) hawapaswi kufuatilia kutawala, kunyanyasana, au kutishana.” Baghaei amejibu matamshi ya Fidan kwa swali, "Lakini vipi kuhusu Israel?"