Qalibaf awatakia kheri ya Ramadhani maspika wenzake katika nchi za Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i123390-qalibaf_awatakia_kheri_ya_ramadhani_maspika_wenzake_katika_nchi_za_kiislamu
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf amewapongeza maspika wenzake katika nchi za Kiislamu kwa kuwasili mwezi mtukufu wa Ramadhani.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Mar 02, 2025 03:26 UTC
  • Qalibaf awatakia kheri ya Ramadhani maspika wenzake katika nchi za Kiislamu

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf amewapongeza maspika wenzake katika nchi za Kiislamu kwa kuwasili mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Qalibaf amesema katika ujumbe wake kwa maspika wa mabunge ya nchi za Waislamu kwamba: “Ninatumai kuwa katika mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu tutashuhudia kuimarika zaidi mfungamano wa udugu na urafiki baina ya mataifa ya Kiislamu na kusimamisha uadilifu na amani ya kudumu duniani kwa kunufaika na mafundisho ya dini yenye nuru ya Uislamu, na kwamba Umma mkubwa wa Kiislamu utaweza kusonga mbele zaidi na zaidi katika njia ya ustawi katika nuru ya umoja na mshikamano wa pande zote.

Mohammad Baqer Qalibaf

Sehemu moja ya ujumbe wa kheri za mwezi Ramadhani za Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu imesema: Hii leo nchi za Kiarabu na Kiislamu zinakabiliwa na mtihani mkubwa, na kadhia ya Palestina ndiyo kipaumbele cha kwanza sio tu cha watu wa eneo hili, bali pia ni nembo ya umoja wa ubinadamu na suala muhimu zaidi la pamoja la Umma wa Kiislamu tangu zamani hadi siku zijazo. Amesisitiza kuwa, stratijia ya Muqawama na mapambano itaendelea kwa nguvu zote hadi kukomeshwa kikamilifu dhulma na uvamizi katika nchi ya Palestina.

Spika Mohammad Baqer Qalibaf ameyahimiza mabunge ya nchi za Waislamu kutekeleza vyema majukumu yao ya kutetea malengo na mapambano ya ukombozi ya watu wa Palestina. 

Mfungo wa mwezi wa Ramadhani umeanza rasmi leo nchini Iran na katika nchi nyingine kadhaa za Kiislamu. Waislamu katika baadhi ya nchi za Kiislamu na Kiarabu walianza mwezi Ramadhani jana Jumamosi.